September 29, 2024

Simulizi ya wananchi wanaopambana kuokoa maisha Geita

Ni wakazi wa Bunigonzi wilayani Mbogwe ambao wamekamilisha ujenzi wa boma la kituo cha afya huku wakisubiri Serikali ikamilishe hatua iliyobaki ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.

  • Wamejenga bomba la kituo cha afya ili kianze kutoa huduma.
  • Ni wakazi wa kata ya Bunigonzi ambao hawajawahi kuwa kituo cha afya.
  • Kitaokoa maisha ya watu wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Mbogwe. Ni mwendo wa saa mbili hivi kwa gari kutoka katika mji mdogo wa Masumbwe wilayani Mbogwe hadi kufika katika kijiji cha Bunigonzi wilayani humo.

Safari ya kufika katika kijiji hicho kilichopo kata ya Bunigonzi itakulazimu kupita katika barabara ya vumbi yenye mashimo yaliyoibuka baada ya mvua kubwa kunyesha mwaka huu.

Kwa wageni, wanaweza kufikiri kuwa ubovu wa barabara ni tatizo kubwa linalowakabili wanakajiji hawa, la hasha. Ni zahanati.

Mashimo? Barabara siyo tatizo

Kwao licha ya barabara kuwa muhimu, huduma za afya ni kipaumbele zaidi kwa kuwa sehemu kubwa wanatumia usafiri wa miguu, baiskeli na pikipiki.

Kinachowaumiza kichwa ni kutokuwa na zahanati kwa ajili ya kupata matibabu pale wanapougua kwa sababu baadhi yao hupoteza maisha na kushindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

“Inafikia hatua wazee na watoto wanapougua inakuwa ni shida kwenda kufika hospitali ya jirani ambayo iko mbali. Ni vigumu kupata msaada pale akina mama wanapopata uchungu usiku…unakuta mama anajifungulia njiani,” anasema Regina Antony mkazi wa kijiji hicho.

Regina anasema hali hiyo imewaondolea wanawake kujiamini na kushindwa kuendelea kutokana na kukosa ulinzi wa afya zao. 

“Na sisi ni watu tunaostahili kupata huduma za kiafya,” anasisitiza mama huyo mwenye watoto wanne ambapo mmoja alijifungulia nyumbani.

Tayari wakazi wa Bunigonzi wamekamilisha ujenzi wa boma la kituo cha afya huku wakisubiri Serikali ikamilishe hatua iliyobaki. Picha| Gift Mijoe.

Wanapoteza ndugu, fedha

Ili waifikie zahanati ya Ushirika iliyopo kata ya Ushirika hulazimika kusafiri umbali wa kilomita nane kwa baiskeli au pikipiki za kukodi kwa kati ya Sh7,000 hadi Sh10,000. Na wasio na fedha hulazimika kutembea kwa miguu ambapo ni mwendo usiopungua saa tano kwa wagonjwa.  

“Mwaka jana, mama mmoja mjamzito alifariki dunia kwa sababu usafiri ulikosekana kumpeleka Ushirika, tukapoteza mama na mtoto,” anasema Allan Ntejo, mhudumu wa afya ngazi ya jamii ambaye amekuwa akitoa msaada wa kwanza kwa wagonjwa kabla ya kupelekwa hospitali. 

Hata hivyo, siyo rahisi kufika katika zahanati hiyo kutokana na ubovu wa barabara na hata wakifika changamoto inabaki kupata huduma kwa wakati kutokana na wingi wa wagonjwa wanaohudumiwa katika zahanati hiyo.

Hali hiyo huwafanya baadhi ya watu kutumia dawa za asili bila kupata vipimo wakihofia gharama za kufika na kupanga foleni kupata huduma katika zahanati ya Ushirika ambayo inahudumia wakazi wa kata tatu ikiwemo Ngemo na Bunigonzi.  

Mhudumu wa Afya katika zahanati hiyo, Luhende Bundala anasema zahanati hiyo inahudumia wagonjwa zaidi ya 60 kwa siku na kwa magonjwa ambayo yako nje ya uwezo wao hutoa rufaa kuwapeleka katika kituo cha afya ambacho kiko mbali na eneo hilo.

                       

Waanza kujenga kituo cha afya

Adha hiyo ya kukosa huduma ya afya iliwasukuma wakazi wa kata ya Bunigonzi kuanza mchakato wa kujenga kituo cha afya kitakachohudumia wakazi wa kata hiyo wanaofikia 7,018.

Ujenzi wa kituo hicho cha afya ulianza mwaka 2017 ambapo baada ya mivutano ya wananchi wamefanikiwa kujenga boma moja wakisubiri Serikali imalizie sehemu iliyobaki ili kianze kutoa huduma. 

Hadi sasa wakazi wa kata hiyo bado wanasubiria kituo hicho licha ya kuwa kina miaka takriban minne tangu kianze kujengwa. 

Mkazi wa kijiji cha Bunigonzi, Maria Welolo anasema wananchi walihamasika baada ya kufundishwa ushiriki katika maendeleo kupitia uraghibishi. 

Anasema mafunzo hayo, yaliyotolewa na asasi ya kiraia ya Tamasha iliyokuwa inafanya kazi kwa karibu wa shirika la Twaweza, yaliwawezesha wananchi kujitambua na kutatua changamoto zao bila kusubiri Serikali. 

“Ujenzi umechukua muda mrefu kwa sababu mara ya kwanza watu walikuwa hawana hamasa lakini walipokuja waraghibishi miaka minne iliyopita wakaamka na wakaanza kujenga kwa nguvu zao,” anasema Maria ambaye ni mraghibishi katika kata ya Bunigonzi. 

Wakati wakazi hao wakisubiri kituo cha afya kianze kufanya kazi, wenzao wa kijiji cha Nyakafuru ambao walikuwa nao katika mafunzo ya uraghibishi wamefanikiwa kujenga zahanati na imeanza kufanya kazi.

“Tulianza mwaka mmoja kujenga zahanati yetu kama wao, lakini sisi tulikuwa na ushirikiano mkubwa na ndiyo maana zahanati yetu imeanza kufanya kazi kwa sababu tuliwabana viongozi wa Serikali wakaleta vifaa na wataalam wa afya,” anasema Rebeka Makenza, mkazi wa kata ya  Nyakafuru wilayani humo.

Eneo la kituo cha afya cha Bunigonzi ambacho kitamaliza changamoto ya wananchi kufuata huduma za afya mbali na eneo lao. Picha| Gift Mijoe.

Kilio chao kitasikilizwa?

Wakazi hao wa Bunigonzi wanasema wamefanya kwa sehemu yao kujenga maboma ya kituo cha afya na Serikali ikamilishe hatua iliyosalia kwa sababu itasaidia kata nzima. 

Diwani wa kata hiyo, Sylivester Ntugwa anasema mpaka sasa wametumia Sh8 milioni kujenga kituo hicho cha afya na kila mwananchi wa kata hiyo alichangia Sh23,000. 

“Kwa sehemu tuliyofikia basi Serikali itushike mkono kwani tumejipiga piga sana. Serikali ituone na sisi kama ni Watanzania tunaiomba itusaidie maana zahanati nyingine zinasaidiwa na zinafanya kazi,” anasema Ntugwa.

Kwa kawaida, wananchi wengi wanatazamia kuiona Serikali ikiwajibika katika ujenzi wa miundombinu ya afya kwa kuwa wanachangia kodi yao kwa ajili ya kuleta maendeleo. Wananchi hao wameamua kuwa tofauti na wanaotegemea Serikali iwaletee kila kitu. 

Huenda mwaka huu, Serikali ikawafuta machozi wakazi wa Bunigonzi kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imesema imetengewa fedha kwa ajili ya huduma za afya katika bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2021/22 ambayo itatoa muelekeo wa kumalizika kwa kituo hicho cha afya.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pastory Mukaruka anasema wananchi wamejenga maboma mengi ya vituo vya afya na Serikali haiwezi kuyakamilisha kwa wakati mmoja.

“Kila mwaka kama Serikali hupunguza au kukamilisha hayo maboma ili yaweze kutoa huduma,” anasema Mukaruka.