November 24, 2024

Siri mikoa saba kutawala matokeo kidato cha pili miaka mitatu iliyopita

Mikoa hiyo ni Arusha, Njombe, Kigoma, Kilimanjaro, Kagera, Shinyanga na Mwanza haijawai kutoka katika 10 bora za mpangilio wa ufaulu kimkoa tangu mwaka 2016.

  • Mikoa hiyo ni Arusha, Njombe, Kigoma, Kilimanjaro, Kagera, Shinyanga na Mwanza haijawai kutoka katika 10 bora za mpangilio wa ufaulu kimkoa tangu mwaka 2016.
  • Wadau wapendekeza utoaji elimu nchini uboreshwe ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa sahihi. 
  • Mikoa nayo yatakiwa kujiwekea mikakati binafsi ili kuongeza ushindani ngazi ya kitaifa.

Dar es salaam. Wakati wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2018 wakivuta subira ya kupata matokeo yao, wadogo zao wamefahamu mbivu na mbichi baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha pili jijini Dodoma Januari 4, 2019. 

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa NECTA, Dk Charles Msonde, alisema wanafunzi 545,077 walisajiliwa kufanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili (FTNA) mwaka 2018, ambapo  wanafunzi 506,235 ndiyo walifanya mtihani huo. 

Takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi 452,273 sawa na asilimia 89.68 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamefaulu kuendelea na masomo ya kidato cha tatu. 

Wakati ufaulu ukiongezeka, bado matokeo hayo yanafikirisha hasa katika mpangilio wa ufaulu kimkoa ambapo Nukta imebaini kuwa mikoa saba imeendelea kutamba katika 10 bora kwa miaka mitatu mfululizo ukilinganisha na mikoa mingine ambayo haijafanikiwa kufanya vizuri. 

Mikoa hiyo ni Arusha, Njombe, Kigoma, Kilimanjaro, Kagera, Shinyanga na Mwanza ambayo haijawai kutoka katika 10 bora za kimkoa tangu mwaka 2016 hadi 2018. 

Katika kipindi hicho, 10 bora ya ufaulu kimkoa kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara imeshikiliwa na mikoa ya Arusha, Njombe, Kigoma, Kilimanjaro, Kagera, Shinyanga, Mwanza, Manyara Iringa, Mbeya, Tabora, Pwani na Simiyu.

Baadhi ya mikoa iliingia na kutoka katika 10 bora hiyo kwa nyakati tofauti kutokana na mchuano mkali uliokuwepo. 


Zinazohusiana:


Mathalani mwaka 2016 mikoa ya Mbeya na Iringa haikufanikiwa kuingia kwenye kundi hilo na mwaka uliofuata wa 2017, Manyara iliondolewa japokuwa mikoa hiyo iliingia mara mbili katika kipindi hicho. 

Manyara ilifanya vizuri 2016 na mwaka uliofuata iliondolewa katika 10 bora lakini katika matokeo ya mwaka huu imerudi tena kwa kasi na kushika nafasi ya 8 kutoka nafasi ya 12 mwaka 2017.  

Mikoa ya Tabora, Pwani na Simiyu yenyewe iliingia mara moja tu, ambapo katika matokeo ya mwaka huu haikufanikiwa kuingia kabisa. 

Mikoa hiyo ni miongoni mwa maeneo nchini ambayo yana mwamko mkubwa wa elimu ukiwemo Kilimanjaro ambao umekuwa ukifanya vizuri katika eneo la kuwapatia wanafunzi chakula wanapokuwa shuleni.

Wakati mikoa hiyo ikitamba katika 10 bora, mikoa ya Lindi, Mtwara, Mara, Tanga, Ruvuma, Katavi, Tabora, Rukwa, Morogoro na Dodoma imeshikilia mkia kwa kuingia katika kundi la mikoa 10 iliyofanya vibaya katika matokeo ya mwaka 2018.


Uboreshaji wa mazingira na njia za ufundishaji utasaidia wanafunzi katika mikoa inayofanya vibaya kupata maarifa sahihi kuwawezesha kujibu mitihani. Picha| Jestina george.

Hali hii inafikirisha ikiwa Tanzania bara yenye mikoa 26 huku mikoa saba ikionekana kuwa vinara katika matokeo ya kidato cha pili kwa miaka mitatu mfululizo, mikoa mingine iko wapi? Kuna siri gani kwa mikoa hiyo saba kutamba 10 bora kwa miaka mitatu mfululizo? 

Wachambuzi wa masuala ya elimu nchini wamesema matokeo ya mpangilio wa ufaulu kimkoa yanachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia katika shule hasa zinazomilikiwa na watu binafsi zilizopo katika mikoa inayofanya vizuri. 

“Matokeo ya namna hii ya mikoa michache kuongoza mara nyingi inachangiwa na mazingira ya shule zenyewe na jitihada za mkoa husika,” anasema Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa.

Jambo lingine ambalo limekuwa likihatarisha ufaulu wa wanafunzi ni umbali kutoka shule hadi nyumbani ambapo baadhi ya mikoa iliyofanya vizuri imekuwa na mikakati mbalimbali ikiwemo kujenga mabweni, kutoa chakula kwa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kutoa matisha kwa walimu. 

“Kuna hata baadhi ya mikoa inaweka makambi ya wanafunzi kabla ya mitihani yote hii ni katika kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri kimkoa,”amesema Dk Mkonongwa.

Mikoa ambayo imekuwa ikifanya vibaya ni vema iige mfano wa mikoa inayofanya vizuri ili kuhakikisha inasimamia utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa maeneo yao.