July 8, 2024

Siri ya Temeke kuandikisha wanafunzi wengi wakike elimu ya msingi

Asilimia 52 ya wanafunzi wote elimu ya msingi wilayani humo ni wasichana na ndiyo inayoongoza kwa udahili wa watoto wakike.

  • Asilimia 52 ya wanafunzi wote elimu ya msingi wilayani humo ni wasichana.
  • Ndiyo halmashauri inayoongoza kwa udahili wa wanafunzi wa kike mkoa wa Dar es Salaam.
  • Wadau washauri nguvu kubwa ielekezwe kwenye kuboresha elimu.

Dar es Salaam.  Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam imefanikiwa katika uandikishaji wanafunzi unaozingatia usawa wa kijinsia katika shule za msingi kuvuka Malengo ya Maendeleo Endelevu ya kutoa elimu bora yenye usawa kabla ya mwaka 2030.

Uchambuzi wa takwimu za uandikishaji wanafunzi wa shule za msingi nchini mwaka 2017 uliofanywa na Nukta umebaini kuwa asilimia 51 ya wanafunzi waliokuwepo wilayani humo walikuwa ni wasichana hivyo kuwa halmashauri inayoongoza kwa uwiano uliovuka lengo la 50 kwa 50.

Kwa muktadha huo, kati ya wanafunzi 100 wa shule za msingi wilayani Temeke, 51 ni wasichana.

Takwimu hizo za Ofisi ya Rais – Tamisemi zilizochapishwa katika tovuti ya takwimu huria ya Open Data zinaonyesha kuwa Shule za msingi 126 katika wilaya hiyo mwaka 2017 zilikuwa na wanafunzi takribani 163,923 huku kati yao wasichana wakiwa ni 83,626 sawa na asilimia 51.

Katika takwimu hizo zilizochapishwa Julai 31 mwaka jana, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke iliongoza kwa udahili wa wasichana ikifuatiwa na Ilala huku Kigamboni ikiwa ya mwisho ikiwa na asilimia 50.2. 

Hata hivyo, halmashauri zote za Dar es Salaam zilikuwa na wasichana wengi kuliko wavulana katika elimu ya msingi na kufanya wastani wa watoto wakike kuwa asilimia 50.7.

Mwenendo huo ulikuwepo hata kabla Temeke haijagawanywa na kuzaa Kigamboni baada ya takwimu za msingi za elimu mwaka 2016 (Best) kuonyesha kuwa wasichana walikuwa asilimia 52 ikiwa ni wengi kidogo kuliko wavulana.

Kutokana na mwenendo wa uandikishaji wanafunzi wa shule za msingi, wilaya hiyo ilishavuka malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu kwa kiwango sawa na wavulana ili kufaidi fursa zilizopo kwa usawa.

Kwanini Temeke idadi kubwa ya wanafunzi wakike?

Ongezeko hilo la udahili wa wasichana si bahati mbaya. Watafiti wanasema huenda sababu za kibaolojia zimechangia ongezeko la watoto wa kike hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kuandikishwa kwa wingi katika shule za msingi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiria kuwa mwaka 2017, wilaya ya Temeke ilikuwa na wakazi milioni 1.5 ambapo wanawake walikuwa 818,765 na wanaume ni 778,714. Hiyo ina maana kuwa katika kila wakazi 100 wa wilaya hiyo, 51 ni wa jinsia ya kike.

Ongezeko hilo la wasichana katika shule za msingi linaweza pia kuwa ni matokeo ya kampeni za kitaifa na kimataifa za kumkomboa msichana na mwanamke kifikra na kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inayosisitiza usawa katika kupata fursa za elimu .

Wanafunzi wa shule ya msingi wakifurahi kwa pamoja. Utoaji elimu kwa usawa unawapa fursa sawa watoto nchini. Picha kwa hisani ya Shirika la The Aga Khan Foundation. 

Pia baadhi ya wadau wameiambia Nukta kuwa utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo katika shule za msingi na sekondari umekuwa ni kichocheo kikubwa cha kuvutia wanafunzi wengi hasa wa kike kwenda shule.

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lulu Mahai amesema sera ya elimu bila malipo imekuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaotoka katika familia masikini kuandikishwa kwa wingi katika shule za serikali lakini changamoto iliyobaki ni ubora wa elimu inayotolewa.


Nini kifanyike kuendeleza 50/50 hadi ngazi za juu za elimu

Wadau mbalimbali wa elimu wamesisitiza zaidi katika utolewaji wa elimu bora inayokusudia kumkomboa mtoto kifikra na kumuongezea maarifa na ujuzi utakaosaidia kuimarisha usawa katika jamii.

Mwanaharakati wa Haki za Watoto, Richard Mabala amesema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia usawa katika uandikishaji lakini jitihada zinahitajika kuongeza ulinzi kwa wanafunzi hasa wa kike ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukatili wa kingono.

“Katika uandikishaji hiyo 50 kwa 50 serikali imefanikiwa. Mimi naamini suala kubwa elimu bure, pili ulinzi kwasababu mimi kama mzazi nikijua shuleni wasichana wanatongozwa, wanatishiwa kubakwa na njiani hakuna ulinzi. Kwahiyo kuwe na ulinzi wa kutosha kuhakikisha watoto wako salama na wanaendelea na elimu ya juu,” anaeleza Mabala.

Mabala anashauri kuitishwa mjadala wa kitaifa kwa sababu bado elimu inayotolewa haina ubora ikiwemo wahitimu wa elimu ya juu kushindwa kufanya hata maswali ya ngazi za chini za elimu.

Kujua shule bora za sekondari mkoa wa Dar es Salaam soma zaidi katika tovuti ya Elimu Yangu

Wanafunzi wakiwa darasani katika moja ya shule za sekondari nchini. Uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia yatasaidia kuwawezesha watoto wakike kufika hadi elimu ya juu kwa kiwango kama ilivyo elimu ya msingi. Picha ya Mtandao.

Mbali na ulinzi wa watoto wa kike, Mtetezi wa Haki za Binadamu kutoka taasisi ya Equity for Growth (EfG) Jane Magigita amesema kuna haja ya kuboresha rasilimali muhimu za elimu kama vifaa, maabara, madarasa walimu, nyumba za walimu. 

“Lazima pia tuhakikishe kuna ofisi nzuri za walimu, vitabu na lishe kwa kuwa imeonekana shule zinapokuwa na chakula watoto wanakaa sana darasani na usikivu wa watoto unakuwa mzuri,” anasema Jane. 

Serikali imeeleza kuwa mikakati mbalimbali ilitumika kufanikisha uandikishaji wenye usawa katika elimu ya msingi na sekondari ikiwemo kuelimisha wananchi umuhimu wa kuwaandikisha watoto wote shule bila kujali jinsia kulikochagizwa na elimu bure.


Mikakati ya Wilaya ya Temeke kuboresha elimu

 “Tumekuwa tukitoa hamasa kwa wazazi kuwapeleka watoto shuleni kupitia mikutano ya serikali za mitaa. Lakini sera ya elimu bila malipo inayotekelezwa na serikali imechangia sana ongezeko la uandikishaji shuleni,” anaeleza Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva.

Lyaniva amebainisha kuwa wazazi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuwapeleka watoto shuleni hasa wa kike ikizingatiwa kuwa wilaya yake imefanya maboresho makubwa ya miundombinu ya shule, madarasa na madawati.

Kiongozi huyo ameiambia Nukta kuwa wanaendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu ikiwemo kuongeza idadi ya shule, madarasa, walimu na vitendea kazi ili kuendana na ongezeko la wanafunzi katika shule na kuhakikisha wanabaki katika nafasi nzuri ya kufikia malengo ya kitaifa na Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

 “Tunaendelea kuboresha mazingira ya elimu ikiwemo maslahi ya walimu, watoto, kujenga madarasa na shule na kutoa hamasa kwa wazazi kuwapeleka watoto shule,” amesema DC Lyaniva.