Spika Ndugai awajia juu Wabunge wanawake kuhusu mirathi
Amewataka wasiisubiri Serikali kuboresha na kutatua changamoto za wanawake bali watumie kanuni za Bunge kuifanyia marekebisho Sheria ya Mirathi sura 352.
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wanaweza kutumia njia mbalimbali zilizopo kwenye kanuni za Bunge kufanya jambo moja litakalowasaidia wanawake kuondokana na unyanyasaji wanaoupata kwenye jamii hasa wajane. Picha|Mtandao.
- Amewataka wasiisubiri Serikali kuboresha na kutatua changamoto za wanawake.
- Wametakiwa kujitathmni walichofanya kuboresha hali za wanawake wa Tanzania.
- Awataka watumie kanuni za Bunge kurekebisha sheria ya mirathi.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka Wabunge wanawake wajitathmini katika muda waliokaa bungeni wamefanya nini kubadilisha hali za wanawake wa Tanzania ikiwemo kuwapatia ahueni ya changamoto ya mirathi na unyanyasaji katika familia.
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo Bungeni leo (Juni 18, 2019) mara baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Augustine Mahiga kueleza hatua ambazo wizara yake inachukua katika kuwasaidia wajane ambao wamefukuzwa katika nyumba za familia zao kupata mirathi.
Mahiga alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Silafu Jumbe Maufi aliyetaka kujua Serikali haioni umuhimu wa kubadilisha sheria ya mirathi ili kumuwezesha mjane kupata haki zake kirahisi ikiwemo mirathi kama ilivyo kwa mgane.
Maufi amesema mgane anapobaki na watoto, hundi zinazolipwa huandikwa kwa jina lake lakini kwa wajane ni tofauti kwani hupewa masharti ya kulipiwa mahakamani na kubainisha kuwa Serikali haioni kama huo ni unyanyasaji?
Baada ya Balozi Mahiga kujibu swali la Mbunge huyo, Spika Ndugai alisimama katika kiti chake na kuwashauri wabunge wanawake kuwa wapeleke muswada bungeni utakaosaidia kurekebisha hali za wanawake na kuacha kuisubiri Serikali iwafanyie kila kitu.
“Swali hili ni muhimu sana kwa TWPG (Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania) , kwa mikutano mitatu iliyobaki nyinyi wabunge wanawake wote msponsor (mdhamini) muswada fulani wa kwenu wenyewe, rekebisheni haya mambo msisubiri Serikali peke yake,” amesema Ndugai.
Amesema wanaweza kutumia njia mbalimbali zilizopo kwenye kanuni za Bunge kufanya jambo moja litakalowasaidia wanawake kuondokana na unyanyasaji wanaoupata kwenye jamii hasa wajane.
Zinazohusiana:
- Bunge lahoji Serikali kutojenga bandari ya Bagamoyo
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Hata hivyo, amewataka wajitathmini kwa miaka mitano ya ubunge wao ambao unaisha mwaka 2020, wamefanya nini katika kuchagiza maisha bora kwa wanawake kwa sababu wao ndiyo wawakilishi wenye sauti katika jamii.
“Ebu fanyeni moja la wanawake, kwa mfano iwe ni marufuku katika nchi yetu mama na familia kufukuzwa katika nyumba ya familia. Kwa mfano tu!.
“Haya mambo ya mirathi wanahangaika kweli, wanateseka na nyinyi ni wabunge wao. Katika miaka mitano mmesponsor (mmedhamini) nini cha kubadilisha hali yao au itaisha hivi hivi tu viti maalum? Tufanye kitu,” amesisitiza Ndugai.
Awali, akitolea ufanunuzi wa suala la mirathi, Balozi Mahiga amesema masuala ya mirathi yanasimamiwa na Sheria ya Mirathi sura 352. Sheria hii inatoa utaribu mzima wa mirathi na wosia wa marehemu.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna sheria yeyote inayompa mgane haki zaidi ya mjane au kwa namna yoyote ya ubaguzi.
Hata hivyo, amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa mkakati mahususi wa kuwalinda na kuwasaidia wanawake waliofiwa na waume zao kupata haki zao bila kusumbuliwa.