Spika Ndugai awatahadharisha Wabunge wanaotumia usafiri wa bodaboda
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewataka Wabunge wanaotumia usafiri wa bodaboda kuingia na kutoka bungeni kuwa makini na madereva wanaowaendesha ili kulinda usalama wao.
- Asema ni usafiri mzuri lakini wanatakiwa kuwa makini na madereva wa bodaboda wanaowaendesha ili kulinda usalama wao.
- Awataka wajiulize wananchi waliowachagua watatafsiri nini wakiwaona wanatumia usafiri huo.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewataka Wabunge wanaotumia usafiri wa bodaboda kuingia na kutoka bungeni kuwa makini na madereva wanaowaendesha ili kulinda usalama wao.
Ndugai aliyekuwa akizungumza leo Aprili 16, 2021 katika kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma amesema usafiri huo ni mzuri na hana shida nao kwa sababu unatumiwa sana na wananchi wakiwemo baadhi ya Wabunge.
“Wako baadhi ya Wabunge wanakuja bungeni kwa usafiri ule mzuri kabisa wa wananchi, usafiri wa bodaboda na kurudi kwa usafiri wa bodaboda,” amesema Ngugai
Hata hivyo, amewataka kuwa makini na kuhakikisha wanawafahamu vizuri madereva wanaowabeba jambo likalowasaidia kulinda usalama wao kwa sababu Serikali inatumia gharama kubwa katika uchaguzi kuwapata wabunge ambao wanaingia bungeni kutunga sheria na kuishauri Serikali katika mambo muhimu ya maendeleo.
“Ni usafiri mzuri sina sida nao lakini basi nawaomba umakini na kuwa na uhakika wa huyo bodaboda maana kupatikana kwenu jamani ni kwa gharama kubwa, nadhani mnanisoma,” amesema Ndugai Bungeni leo jijini Dodoma huku baadhi ya Wabunge wakitabasamu.
Zinazohusiana:
- Tusipowasaidia, Tanzania itawapoteza bodaboda wote
- Lugola ataja bodaboda wanaopaswa kupelekwa polisi
- CHATI YA SIKU: Bajaj, Bodaboda zinavyoangamiza watu Tanzania
Aidha, amewataka wabunge hao wanaotumia usafiri huo kujiuliza wananchi waliowachagua watatafsiri nini wakiwaona viongozi wao waliowachagua wanatumia usafiri wa bodaboda kwenda bungeni.
“Pia ni vizuri kuelewa wananchi wakikuona huko watatafsiri vipi,” amesema Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma.
Usafiri wa pikipiki wa magurudumu mawili maarufu kama bodaboda umekuwa ni msaada mkubwa wa usafiri katika maeneo mengi yasiyokuwa na usafiri wa uhakika nchini. Mbali na kutoa huduma za usafiri, bodaboda zimetoa ajira kwa vijana wengi.
Hata hivyo, usafiri huo umekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani kutokana na baadhi ya madereva wake kutozingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo mwendo kasi, kutokuvaa kofia ngumu na matumizi ya pombe.