November 24, 2024

Statoil yaja kivingine uchimbaji wa gesi Tanzania

Statoil yasema mabadiliko ya jina hayataathiri shughuli za uchimbaji gesi nchini

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Equinor duniani Eldar Sætre akitambulisha jina jipya la Statoil Mei 16 mwaka huu. Picha|NTB Scanpix

  • Statoil yasema mabadiliko ya jina hilo hayataathiri shughuli za uchimbaji gesi nchini.
  • Ni mpango wa kujitanua katika sekta ya nishati duniani.
  • Equinor inalenga zaidi kwenye usawa, haki na mlinganyo wa nishati.

Dar es Salaam. Kampuni ya Statoil imebadilisha jina na sasa inaitwa Equinor ASA ikiwa ni njia ya kuboresha huduma zake na kujitanua kwenye soko la ushindani wa ugunduzi na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini. 

Mabadiliko hayo yanahusu pia matawi yote ya kampuni hiyo yaliyopo duniani likiwemo la Statoil Tanzania AS ambayo sasa inajulikana kama Equinor Tanzania AS.

Taarifa kwa umma ya kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake nchini Norway inaeleza kuwa mabadiliko yaliyofanyika hayatagusa mfumo wa utawala, umiliki na maswala ya kisheria na shughuli zingine za uzalishaji zitaendelea kuratibiwa kama awali.

“Tunataka umma uelewe kuwa mabadiliko ya jina letu: mikakati, tunayosimamia (Uwazi, ushirikiano, ujasiri na kujali), utendaji na mwelekeo wetu wa kuendeleza rasilimali zilizogunduliwa katika kitalu namba 2 kwenye mwambao wa Tanzania utabaki kama kawaida,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa leo (Agosti 13, 2018). 

Uamuzi huo ni matokeo ya mkutano mkuu uliofanyika May 16, 2018 wa kampuni ya Statoil Group ambayo ni kampuni mama ya Statoil ASA ili kuhakikisha inatumia jina linaloendana na mabadiliko ya teknolojia ya uendelezaji wa nishati. 

“Equinor ni jina pana linaloangazia nyanja zote za biashara yetu ya mafuta, gesi na nishati jadidifu ambayo inajumuisha umemejua na upepo.” inafafanunua sehemu ya taarifa hiyo kwa umma.

Mapendekezo ya jina jipya la Equinor siyo ya bahati mbaya kwa mujibu wa Equinor. ‘Equi’ ambacho ni kianzio cha jina hilo kinamanisha usawa ikiwa au mlinganyo ikiwa na maana ya maono mapya ya kampuni hiyo inavyowatazama watu na nishati kwa ujumla. 

Sehemu ya mwisho ya ‘Nor’ inasadifu chimbuko la kampuni hiyo kutoka Norway iliyoanzishwa mwaka 1972  na kusambaa katika nchi 34 duniani ikijihusisha na uchimbaji na uendelezaji wa rasilimali asilia ikiwemo gesi na mafuta na matumizi ya nishati mbadala ya upepo na jua. 

Moja ya mitambo ya kuchimba mafuta baharini inayomilikiwa na Equinor. Picha| Spash247.com.

Statoil ASA ambayo sasa ni Equinor Tanzania AS iliingia Tanzania mwaka 2007 kwa makubaliano ya uzalishaji wa ubia (Production Sharing Agreement) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili uendelezaji kitalu namba 2 cha gesi kwenye mwambao wa bahari ya Hindi kilichopo mkoa wa Mtwara. 

Katika makubaliano hayo Equinor ina hisa za asilimia 65 huku kampuni ya ExxonMobil ikimiliki asilimia 35 na TPDC inaweza kuingia kwenye leseni kwa asilimia 10 ikiwa thamani ya biashara ya gesi itathibitika. 

Equinor ambayo ofisi zake ziko jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na ExxonMobil wamegundua gesi inayofikia futi za ujazo 23 chini ya bahari ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuongeza Pato la Taifa (GDP) na kukuza wigo wa biashara ya gesi katika nchi zingine za Afrika Mashariki. 

Kwa mujibu wa Equinor tangu mwaka 2010 hadi 2017 imewekeza Dola za Marekani 2.1 bilioni katika shughuli zake na kuajiri wafanyakazi 30 ambapo wamefanikiwa kutoa mafunzo ya rasilimali asilia kwa watu zaidi ya 500 kutoka kwenye sekta binafsi na umma.