October 6, 2024

TAA ilivyojipanga kusimamia jengo jipya la abiria uwanja wa ndege wa kimataifa Dar

Tayari imetoa mafunzo kwa wafanyakazi na majaribio ya ndege na kusaini mikataba na watoa huduma mbalimbali.

  • Tayari imetoa mafunzo kwa wafanyakazi na majaribio ya ndege.
  • Imesaini mikataba na wato huduma, imeajiri wafanyakazi watakaosimamia kazi mbalimbali.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha ufanisi wa jengo la tatu la abiria la  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikiwemo kukamilisha mikataba ya watoa huduma katika jengo hilo. 

Jengo hilo maarufu kama Terminal 3 ambalo ni jipya limezinduliwa leo (Agosti 1, 2019) na Rais John Magufuli  baada ya mchakato mrefu wa kulijengwa ulioanza tangu mwaka 2013.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Julius Ndiyamkama amesema wamekamilisha mikataba ya watoa huduma 18 kati ya 27 katika jengo hilo ambapo baadhi yao wameanza kufanya maandalizi. 

Mamlaka hiyo pia imekamilisha kandarasi 22 kati ya 34 ambazo zitahusisha usafi, uangalizi wa mifumo na mitambo katika jengo hilo kuhakikisha usalama wa wasafiri unakuwepo wakati wote.

“Sektretalieti ya utumishi imekamilisha ajira za vijana 130 kati ya 241 waliokua wanahitajika ambao wamesharipoti na baadhi yao wameanza kazi katika jengo la tatu na wengine wakiwa katika mafunzo ya awali ya kuwawezesha kuanza kazi,” amesema Ndiyamkama.


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, Ndiyamkama amesema wametoa mafunzo ya majaribio ya mifumo ya miundombinu ya ndege kwa wafanyakazi ili kuhakikisha ufanisi unakuwepo wakati wa utoaji wa huduma katika jengo hilolinaloweza kuhudumia watu 2,800 kwa saa. 

“Programu hii imeenda vizuri, sisi wenyewe tunajiona tuko tayari, mashirika ya ndege yameridhika na kiwango cha maandalizi na waliohamishia shughuli zao katika jengo jipya ni jumla ya mashirika 18 kati ya mashirika 23 ya safari za kimataifa yaliyopo katika jengo la pili,” amesema.

Jengo hilo litakuwa linafanya kazi sambamba na majengo mengine mawili ya Terminal 3 na Terminal 1 ili kukidhi mahitaji ya wasafiri wanaotumia uwanja wa JNIA. 

“Katika kupunguza msongamano katika kiwanja cha ndege cha kwanza, ndege zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 18 ambazo kwa sasa zipo sita kwa upande ule, zitahamishiwa katika jengo la pili,” amesema.