October 6, 2024

Tabia tano kukuhakikishia afya bora kuendeleza biashara yako

Ni pamoja na kula mlo kamili, kufanya mazoezi, kuacha uvutaji na unywaji wa pombe uliopitiliza na kuepuka unene uliopitiliza.

  • Ni pamoja na kula mlo kamili, kufanya mazoezi, kuacha uvutaji na unywaji wa pombe uliopitiliza na kuepuka unene uliopitiliza. 
  • Afya ndio mtaji namba moja wa kazi au biashara yako, wekeza katika afya ili ufanikiwe. 

Afya ni mtaji namba moja katika kazi au biashara yako. Kama afya inayumba huwezi kutimiza majukumu yako kikamilifu ili kupata mafanikio yaliyokusudiwa katika eneo unalofanyia kazi. 

Sababu kubwa ni kuwa utatumia pesa na muda mwingi kutafuta matibabu  na wakati huo huo mipango yako ikisimama.  

Kwa kiasi gani umewekeza kuboresha afya yako? Hali uliyonayo sasa itakuwezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa familia na Taifa? 

Kama bado una wasiwasi juu ya afya yako, usihofu kwani mabadiliko ya tabia yatakuwezesha kuwa imara wakati wote na kukusaidia kuishi maisha marefu ili mipango yako iende kama ilivyopangwa. 

Ni muhimu kufahamu kuwa msingi wa afya bora ni kubadilika kitabia yaani kuacha baadhi ya vitu ambavyo ni hatarishi kwa afya yako na kuchukua hatua muhimu kufuata ushauri wa wataalam wa afya. 

Karibu wataalam wote wa afya duniani wanakubaliana na tabia tano zinazotakiwa kutekelezwa na mtu ili kuwa na afya bora:

Mlo kamili ni kila kitu

Unatakiwa kula mlo kamili. Hapa ina maana kuwa kula vyakula vyenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini kulingana na ukubwa wa mfuko wako. Zaidi unasisitizwa kula matunda na mboga mboga na epuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi hasa ya wanyama.

Kwa mujibu wa ripoti ya afya ya akili kutoka Chuo Kikuu cha Harvard cha Uingereza ya mwaka 2017 inaeleza kuwa  mlo kamili utakulinda dhidi ya magonjwa nyemelezi na kukuongezea afya ya akili ambayo inahitajika katika utendaji wa kila siku wa biashara yako. 

Chakula chenye virutubisho muhimu ni kinga dhidi ya magonjwa katika mwili lakini kinasaidia kuboresha afya ya akili inayohitajika katika uzalishaji mali. Picha|K15 Photos.

Fanya mazoezi

Mazoezi ni kinga nyingine inayosaidia mwili uwe na mwonekano mzuri na kuchangamsha akili. Bila mazoezi utasikia umechoka na uvuvi utaingia mwilini na matokeo yake ufanisi wa kazi utapungua. Unashauriwa angalau utembee au kukimbia kwa dakika 30 kwa siku.

Kwa mujibu wa Jarida la Afya ya Akili la Marekani linaeleza kuwa mazoezi yanasaidia kuondoa mkazo, msongo wa mawazo na kuufanya ubongo kufanya kazi vizuri, jambo linaloweza kuongeza kasi ya utendaji wa akili inayohitajika katika shughuli za uzalishaji mali.

 

Punguza kupiga ulabu 

Epuka unywaji wa pombe uliopitiliza. Licha ya baadhi ya watu kupendekeza kunywa pombe kiasi lakini unakumbushwa kuwa pombe siyo nzuri kwa afya yako kwasababu ni kichocheo cha magonjwa ya moyo na saratani. 

Lakini ukiendekeza pombe unakuwa teja (addicted) na upande pili hutaweza tena kufanya kazi au biashara jambo linaloweza kukuletea umasikini wa kipato.

Sambamba na hilo epuka uvutaji wa sigara. Wavuta sigara wanatakiwakuacha kabisa kuvuta badala ya kupunguza uvutaji ili kuepuka hatari ya magonjwa ya moyo, mfumo wa upumuaji nakiharusi. 

Utakapoumwa kwa sababu ya matumizi ya pombe na sigara itakulazimu utumie fedha nyingi kupata matibabu ambazo zingetumika katika shughuli nyingine za uwekezaji na biashara. 


Zinazohusiana: 


Mwisho ni kuepuka unene uliopitiliza. Kila umri wa binadamu una kiwango chake za uzito. Baadhi ya mambo yanayochangia unene uliopitiliza ni ulaji mbaya wa chakula nakutokufanya mazoezi. 

Madhara yake unajiweka katika hatari ya kupata  magonjwa ya moyo, kisukari na kushindwa kufanya majukumu ya uzalishaji mali kikamilifu.

Wakati ukifikiria kuwa na bima ya afya au kutafuta pesa za matibabu, basi fikiria jinsia ya kujikinga dhidi ya tabia zisizofaa kwa afya yako. 

Hiyo itakusaidia kuokoa pesa na muda utakaotumia kwenda hospitali badala yake itakupa fursa ya kufanya biashara na kusonga mbele kimaisha.

Hata hivyo, mabadiliko ya tabia ni ya mtu binafsi kwasababu maisha ni kupanga na kuchagua.