November 24, 2024

Tabia zinazowaangamiza vijana mahali pa kazi

kuna tabia mashuhuri ambazo hufanya vijana wengi kupoteza mwelekeo katika kazi zao hususan mahala pa kazi ikiwemo uvivu, dharau na kutojiongeza kitaaluma.

  • Dharau huvunja ushirikiano kazini na hutengeneza maadui.
  • Wavivu wengi hawafikii malengo yao na hata wakifikia basi ni kwa kuunga unga.

Kila kijana anataka kufanikiwa maishani kwa kila kitu anachokifanya. Wengi hupenda tufikie katika ngazi za juu katika kazi zetu au tupate faida ya juu zaidi iwapo tumejikita kufanya biashara.

Hata hivyo, si vijana wote hufikia malengo. Wapo vijana wenye akili nyingi lakini hushindwa kufikia mafanikio wanayoyataka na hata wakati hutengwa na jamii. Wapo pia wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo wa kiakili hufanikiwa zaidi.

Baadhi yetu wametokea familia duni lakini wakafanikiwa zaidi maishani kuliko waliotoka familia zenye ukwasi. Vivyo hivyo, wapo waliotoka katika familia za kitajiri wamefanikiwa kwa yale wanayofanya katika kazi zao kuliko hata waliotoka kwenye maisha duni.

Utofauti huo wa mafanikio katika kazi zetu au taaluma zetu ni matokeo ya mambo katika maisha kuanzia malezi katika familia zetu, mfumo wa jamii na tabia binafsi za vijana.

Licha ya kuwepo sababu lukuki katika hili, kuna tabia mashuhuri ambazo hufanya vijana wengi kupoteza mwelekeo katika kazi zao hususan mahala pa kazi.

1. Dharau

Kwa kuwa wewe ni kijana na unafahamu mambo kutokana na Mungu alivyokujalia unaona umebeba dunia. Unadharau bosi wako kwa sababu hawezi kutumia vizuri programu fulani ya kompyuta iliyoanzishwa kwenye shirika lenu. 

Kwa kuwa unajua Kiingereza unadharau wafanyakazi wenzio ambao hawawezi. Tabia hii ya kudharau vitu au watu huchangia kudumaza vijana kwa kuwa hujiona wamefika na kushindwa kujiongeza.

Dharau huvunja ushirikiano kazini na hutengeneza maadui. Matokeo ya dharau ni kiburi ambacho ni kaburi la kitaaluma na kimaisha kwa vijana wengi sana.

Hata hivyo, siyo vijana wote hufikia malengo. Wapo vijana wenye akili nyingi lakini hushindwa kufikia mafanikio wanayoyataka na hata wakati hutengwa na jamii. Picha|NESA by Makers/Unsplash.

Mara nyingi vijana wenye dharau hata kama ni “smart” bado hujikuta hawakui ipasavyo katika maisha yao. Huwezi kupandishwa cheo kuwa kiongozi kama unadharau. Huwezi kuwa na wateja wengi au washirika wengi wa kibiashara kama unadharau. Dharau inaua ndoto.

 

2. Kutojiongeza kitaaluma

Katika mazingira ya sasa mambo yanabadilika kwa kasi. Baadhi ya ujuzi uliokuwa nao jana kama nguzo muhimu katika kazi zako unaweza usiwe na umuhimu tena. Teknolojia imefanya wafanyakazi kujiongeza kitaaluma na kiujuzi kila siku. 

Hata hivyo, kuna baadhi ya vijana hawajiwekei muda wa kujisomea au kutafuta mafunzo zaidi ili kuimarisha taaluma zao jambo linalowafanya wapoteze thamani kila siku kazini. 

Vijana wengi wa namna hii licha ya kuwa damu bado inachemka, huwa wa kwanza kuondolewa kazini kwa kuwa hawaongezi thamani yeyote katika taasisi pale inapotokea kuna upunguzaji wa wafanyakazi.

Ili kudumu na kukua vyema kitaaluma, ni vema vijana wakajiongeza kimaarifa kwa kutafuta mafunzo ya mtandaoni ya bure ama ya kuyalipia kidogo. Jitihada za namna hii huziba mwanya wa maarifa hasa pale mashirika wanayofanyia kazi yanaposhindwa kugharamia mafunzo. 


Zinazohusiana: 


3. Uvivu

Mara nyingi uvivu ni tabia inayoua ndoto za vijana wengi ulimwenguni. Uvuvi unajengwa na mhusika na zao la muda mrefu. Inaweza kuwa akiwa mtoto alilelewa katika mazingira ya kujituma zaidi kwa kushurutishwa na wazazi lakini kadri umri unavyoenda anazidi kutepeta.

Kwa sasa kuna malalamiko mengi miongoni mwa viongozi wa mashirika wakiwemo niliobahatika kuzungumza nao wanaosema kuwa vijana tumekuwa wavivu sana. 

Kazi iliyotakiwa kufanywa kwa nusu saa, baadhi yetu hufanya kwa saa nzima hadi mawili. Hakuna ari tena ya kufanya vitu kwa ustadi na kwa haraka. Matokeo yake wavivu wengi hawafikii malengo yao na hata wakifikia basi ni kwa kuungaunga tu. Tabia hii ya uvuvi humfanya kijana kuwa hatarini kupoteza kazi yake au kuzika kabisa ndoto zake hata kama amejiajiri.

Ili kutokomeza tabia hii, vijana tunatakiwa kujipangia malengo binafsi yanayorandana na kazi zetu ili kuhakikisha tunayafanikisha. Weka mpango wa kuwahi mapema mahali pa kazi, fanya kazi kwa wakati na jenga mazoea ya kuhakiki maendeleo yako kila siku.

4. Kukata tamaa mapema

Kuna vijana wengi smati kichwani lakini wana roho ya karatasi. Kwa kuwa ni tabia ya kila mwanadamu kunuia mafanikio, pale inapotokea mambo yameenda sivyo, vijana hawa hufa mioyo. Tabia ya kukata tamaa imechangia vijana wengi kutofikia malengo yao.

Mafanikio yoyote yanahitaji uvumilivu. Uvumilivu humfanya mtu kuwa na uzoefu na jambo fulani. Tofauti na miaka ya nyuma, vijana wa sasa wakionywa mara kwa mara na mabosi zao pengine kutokana na uzembe wao, mara nyingi hukata tamaa na kutishia kuacha kazi.  

Tabia ya kukata tamaa imechangia vijana wengi kutofikia malengo yao na kuwaweka katika hatari ya kupoteza kazi. Picha| Tran Mau Tri Tam/Unsplash.

Kuacha kazi au kufunga biashara kutokana na ugumu unaopitia kwa muda mfupi, si suluhu ya kudumu. Sisemi uvumilie mateso au manyanyaso, la hasha, hatua kama hizo huchukuliwa mwishoni baada ya kujiridhisha aina shida unayopitia haivumiliki, haitaisha hivi karibu na ni hatari kwa maisha yako.

5. Ufitini

Kuna vijana wanaamini ili watoboe ni lazima wafanye ufitini fulani kuwaharibia wengine. Mara nyingi tabia hii hufanywa kwa malengo ya kushawishi bosi au mteja awaone wao ni bora kuliko wale wanaowafitini. 

Jambo ambalo wengi hawafahamu ni kuwa ukipata kwa ufitini na utapoteza kwa ufitini. Umbea na kuwasema watu vibaya ili kupata mafanikio hasa katika mahali pa kazi au biashara hakutawafanya vijana kuwa bora.

Vijana ambao huzingatia misingi ya utu, heshima na kurekebishana, hawana tabia ya ufitini na huwashauri wenzao ili wasiharibikiwe hata kama ni washindani wakuu. Ufitini ni matokeo ya kutokuwa na njia bora ya kushirikiana kama timu au wafanyabiashara. Achana na ufitini hautafanya uwe bora.

Kesho tutaangazia namna tabia za kujimwambafai, upotevu wa muda na nyingine zinavyoua vipaji na ndoto za vijana wengi.