Tafakuru yangu kuelekea mwisho wa mwaka 2020
Nakukumbusha juu ya kuijali afya yako utakapoanza mwaka mpya kwa kufanya mazoezi, kula vizuri, pima afya kila inapobidi na fuata maelekezo ya daktari.
- Ni kukumbusha juu ya kuijali afya yako utakapoanza mwaka mpya.
- Hakikisha unazingatia tahadhari za kuwa na afya bora.
- Fanya mazoezi, kula vizuri, pima afya kila inapobidi na fuata maelekezo ya daktari.
Katika makuzi yangu utotoni nilibahatika kuwa mfaidika wa hekaya na hadithi ambazo babu na bibi ama ndugu walitusimulia mara kwa mara kwa lengo la kutuburudisha, kutufunza na kutuonya.
Utamu wa hadithi hizi huingia shubiri pale inapokua inakaribia mwisho. Kwani wakati huo unakua na hamu kubwa ya hadithi hiyo kuendelea au kufahamu mwisho wake utakuaje.
Uchungu wa kufikia tamati kwa hadithi ni funzo kuwa hakujawahi kuwa na marefu yasio na ncha. Tafakuri yangu inanitia mashaka kidogo kama kuisha kwa mwaka 2020 kunawapa watu uchungu wa aina yeyote ile. Ninachelea kusema furaha ya watu kuumaliza mwaka huu ni kubwa kuliko.
Si nia yangu kujaza kibuyu na maneno makavu na siasa hizi, la hasha! Tafakuri yangu inanileta kulikunjua jamvi la masuala ya afya yatakayokuwezesha wewe kujitathmini na kujipanga na mwaka mpya ujao.
Ugonjwa hauna hodi, huja kama mwizi. Lakini uimara wa boma lako humuwazisha mwizi huyu mara mbili mbili kabla ya kufanya uvamizi.
Aghalabu, hata ikiwa amefanikiwa kuingia, atakumbana na upinzani mkali. Hivi ndivyo, miili yetu na kinga yake ilivyojengeka. Kinga ya mwili haijengwi ndani ya usiku mmoja. Wahenga husema Roma haikujengwa usiku mmoja.
Kinga ya mwili ni matokeo ya lishe bora, ufatiliaji wa afya pamoja na ufanyaji wa mazoezi. Ulaji wa matunda yenye vitamini C ya kutosha, mbogamboga pamoja na mlo uliopangiliwa utakuwezesha kuwa na afya bora yenye ustahimilivu dhidi ya magonjwa nyemelezi.
Usikubali kuishi kwa mazoea mwaka 2021. Weka malengo yatakayokusaidia kulinda afya yako ili utimize ndoto zako kikamilifu. Picha|Unsplash.
Saratani zimekua janga kubwa. Saratani haina chanzo maalum. Ni mchanganyiko wa tabia, mazingira na mifumo hatarishi. Lakini gharama zake ni kubwa na hugharimu viungo hadi uhai.
Changamoto kubwa ya saratani huja pale inapokua imegundulika muda ukiwa umeenda. Matibabu huwa ni magumu na uwezekano wa kupona ni mdogo sana. Nini kifanyike?
Jitahidi kufuatilia afya yako kwa ukaribu hasa pale unapoona dalili kama maumivu yasioelezeka, uvimbe nk. Jitahidi kufuatilia upimaji wa afya yako ikiwemo upimaji wa saratani za shingo ya kizazi pamoja na tezi dume.
Saratani hizi huwa na kampeni za upimaji za mara kwa mara. Hii itakuweka kwenye mpango mzuri wa kutambua afya yako.
Usugu wa dawa nao ni janga
Usugu utokanao na matumizi yasio sahihi ya dawa za antibaiotiki umekua chanzo kikubwa cha kushindwa kupata matibabu sahihi wakati unapohitajika. Kumekua na utaratibu wa watu kutumia dawa za antibaiotiki bila maelekezo ya daktari.
Tunaenda mbali zaidi kwa kujitibu magonjwa yasio ya kibakteria kama mafua kwa kutumia dawa hizo.
Hali hii imesababisha usugu mkubwa wa dawa na kuwapa wauguzi na madaktari wakati mgumu wanapokua wakitibu wagonjwa. Hali hii haifai na haina budi kukomeshwa. Usitumie dawa bila maelekezo ya daktari na unapopewa dawa hakikisha unamaliza dozi kwa wakati uliopangwa na kutoishia njiani.
Soma zaidi:
- Zawadi unazoweza kuwanunulia wazazi msimu wa sikukuu
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu “Boxing Day”
- Zawadi za kielektroniki unazoweza kumpatia umpendae msimu wa sikukuu
Corona imetuachia funzo
Janga la Corona limetupa tafakuri kubwa. Limetukumbusha kuwa afya ni muhimu. Lakini somo kubwa likiwa umuhimu wa kuzingatia taarifa sahihi za afya, ufuatiliaji wa afya zetu na utayari wetu wa kupambana na magonjwa. Kuna mengi ya kubadili tunapoelekea mwaka mpya wa 2021.
JIPENDE! NARUDIA TENA JIPENDE! Hakuna mtu atakayependa mwili wako zaidi yako. Magonjwa yasio ya kuambukiza (NCD) yanashika kasi na hii hutokana na watu kutoipenda miili yao na afya zao.
“USIPOKULA CHAKULA KAMA DAWA, UTAKULA DAWA KAMA CHAKULA” na utaukumbuka umuhimu wa kuipenda afya yako ukiwa katika kitanda cha hospitali. Habari njema ni kwamba hauwezi fika huko.
Ufanye nini 2021?
Ukizingatia uzito wako, aina ya vyakula unavyokula na mazoezi pamoja na upimaji wa afya mara kwa mara utajiweka kwenye ramani ya afya bora kila wakati.
Ninakutakia kila la heri katika safari yako kiafya. Kila la heri unapoanza mwaka wa 2021 panapo majaaliwa. Mwenyezi Mungu akubariki sawa sawa na wingi wa fadhili zake. Ni matumaini yangu tutakutana kwenye jukwaa hili tena tukiwa wazima na bukheri wa afya tele.
Nipo!!
Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.