October 8, 2024

Taharuki ya virusi vya Corona italeta maafa zaidi isipodhibitiwa

Wananchi wanakumbushwa kutumia vyanzo vya uhakika kupata taarifa za Corona ili kuepuka taharuki na wanatakiwa kuchukua tahadhari ya kunawa mikono mara kwa mara, kutumia tishu wakati kukohoa nayo inasaidia.

  • Wananchi wanakumbushwa kutumia vyanzo vya uhakika kupata taarifa za Corona ili kuepuka taharuki.
  • Kuchukua tahadhari ya kunawa mikono mara kwa mara, kutumia tishu wakati kukohoa nayo inasaidia.
  • Kubali kuwa Corona ipo ili kuruhusu maisha yaendelee. 

Ugonjwa wa corona unaosababishwa na kirusi aina  ya COVID-19 kama yalivyo magonjwa mengi ya virusi hauna tiba.  Februari 16 2020 Wizara ya Afya ilithibitisha uwepo wa mgonjwa wa kwanza nchini Tanzania. 

Lakini kikubwa ninachotaka tukiangalie ni ukubwa wa tatizo ukilinganisha na ukubwa wa taharuki inayokuja na taharuki yenyewe. 

Nachelea kutumia maneno mengi ya kisayansi kuelezea namna ugonjwa huu unavyomuathiri mwanadamu na kuleta madhara. Nataka tuangalie kwa pamoja athari ya taharuki katika kupambana na ugonjwa huu.

Corona haina tiba lakini mgonjwa anapogundulika kinachotibiwa ni zile dalili zinazokuja na ugonjwa. Sanjari na hayo japokuwa corona ya COVID-19 ina kiwango kikubwa cha maambukizi, lakini kiwango chake cha kusababisha kifo ni kidogo ikilinganishwa na jamii zingine za virusi vya corona. 

Hii humaanisha ya kuwa uimara katika udhibiti wa maambukizi na kujikinga dhidi ya kupata maambukizi ya corona kwa kufata maelekezo ya wataalam wa afya itakusaidia wewe kujikinga zaidi. 

Wahanga wengi ni wazee na watu wenye uimara mdogo wa kinga ya mwili, hii husababisha miili yao kuelemewa na ugonjwa na umauti. Kimsingi huchukua takribani siku saba hadi 10 kwa mgonjwa wa corona kupata nafuu chini ya uangalizi.

Taharuki ni hali ya kawaida na ya kibinadamu kabisa hasa panapokuwepo na tatizo lenye ukubwa kama hili. Lakini taharuki isipodhibitiwa na kuwepo kwa utulivu husababisha  madhara na kushindwa kudhibiti tatizo lenyewe.

 Hali ya taharuki huathiri uwezo na uthabiti wa kufikiria, kusikiliza, kufuatilia na hata kufanya maamuzi. 

Taarifa zinapotolewa kuhusu namna ya kujikinga ili kudhibiti maambukizi zinashindwa kujipenyeza na kutiliwa maanani sababu kubwa ikiwa ni taharuki. 

Na hata watu wakifanikiwa kuzisikia bado utekelezaji wake unakua ni hafifu kutokana na mzio wa taharuki. Matokeo yake ni taharuki inayoleta madhara kuliko hata ugonjwa wenyewe. 

Taharuki hii hupelekea uwepo wa taarifa zisizo rasmi kuhusu ugonjwa huu kupitia mitandao na hata jumbe za simu. Nimeona video kadha wa kadha watu wakikiri kuwa na tiba na wengine wakitoa maelezo yasio na mashiko kitaalamu. Upotofu huu huchochea taharuki kubwa zaidi na kuondoa hali ya utulivu.


Zinazohusiana


Ni muhimu kuzingatia mambo haya matano kwa sasa

Osha mikono mara kwa mara kwa usahihi na kwa maji na sabauni. Unaweza kutumia kitakasa mikono (hand sanitizers) chenye alcohol (kiwango cha pombe) asilimia 60 au zaidi.

Tumia tishu au kiwiko cha mkono wako wakati wa kukohoa au kupiga chafya. Sambamba na hilo usiguse macho, pua na mdomo. 

Epuka misongamano na mikusanyiko ya watu wengi. Jitahidi kukaa mita moja au zaidi ya hapo. Ikiwezekana kaa nyumbani.

Unapohisi kuuma homa kali, mafua, kikohozi, kifua kubana jitengene na jamii na nenda hospitali moja kwa moja ukapate vipimo. Kumbuka siyo kila aliye na mafua ua kikohozi ana virusi vya Corona.

Taharuki huleta maafa zaidi isipodhibitiwa, hivyo ni vyema kufuatilia taarifa rasmi kutoka kwenye vyombo vya habari na shirika la afya duniani (WHO)  pamoja na Wizara ya Afya.

Kamwe usisadiki taarifa au maelekezo yasiyo rasmi au kushiriki katika  kusambaza taarifa hizi. Utaongeza taharuki na maafa zaidi.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.