November 24, 2024

Takukuru yafanikiwa kumnasa kigogo wa TPA aliyetoweka kwa miezi tisa

Hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru mkoani Mwanza (Takukuru) imefanikiwa kumkamata aliyekuwa Mhasibu wa bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka baada ya kumtafuta kwa takribani miezi tisa.

  • Ni Mhasibu wa bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka ambaye hajaonekana kwa takriban miezi tisa.
  • Yeye na wenzake wanatuhumiwa kwa rushwa,  uhujumu uchumi na ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh153 milioni. 

Mwanza. Hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Mwanza (Takukuru) imefanikiwa kumkamata aliyekuwa Mhasibu wa bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka baada ya kumtafuta kwa takribani miezi tisa.

Mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa watuhumiwa wengine watano waliokamatwa na kufikishwa mahakamani wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa,  uhujumu uchumi na ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh153 milioni. 

Mkuu wa Takukuru mkoani Mwanza,  Frank Mkilanya amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa  tangu mwezi Agosti mwaka jana na kuwa amepatikana katika mtaa wa Nyasaka wilayani Ilemela mkoani humu. 

“Mtuhumiwa huyu alikuwa akitafutwa kwa takribani miezi tisa ili aunganishwe na wenzie ambao tayari walifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma tangu Tarehe Agosti 31, 2020,” amesema  Mkilanya.


Zinazohusiana:   


Washtakiwa wengine ni pamoja na Rodrick  Mgwiso aliyekuwa Meneja wa Bandari Kigoma,  Afisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Herman Shimbe,  Mhasibu wa TPA, Jesse Mpenzie (Mhasibu mkazi TPA Kigoma) na Afisa Rasilimari Watu wa TPA Kigoma,  Rusubusyo Mwakyusa

Wakati watuhumiwa hao walipofikishwa mahakamani, Madaraka hakuwepo kwa sababu alikuwa ametoroka na sasa ataunganishwa na wenzake ili kuendelea na mashtaka yanayomkabili.