September 29, 2024

Tamisemi yaweka wazi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano 2021

Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu ametangaza orodha ya watahiniwa 148,127 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa shule za Serikali na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi mwaka 2021.

  • Watahiniwa 148,127 wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi mwaka 2021. 
  • Kati yao, 87,663 wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano.
  • Wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa Julai 3 hadi 18, 2021. 

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu ametangaza orodha ya watahiniwa 148,127 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa shule za Serikali na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi mwaka 2021. 

Kati ya wanafunzi hao, 87,663 sawa na asilimia 59.2 ya wenye sifa wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule 476 za Serikali zikiwemo shule mpya 42.

Waziri Ummy aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni Mosi,  2021 amesema watahiniwa waliochaguliwa ni wale waliokidhi vigezo vya ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne wa mwaka jana.

Amesema katika mtihani huo watahiniwa waliopata daraja la I hadi la III walikuwa 153,464 wakiwemo wasichana 67,135 sawa na  asilimia 35.06 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani huo.

“Baada ya kufanya uchambuzi ambao wamekidhi vigezo na wana sifa za msingi za kuchaguliwa kidato cha tano na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi ni 148,127  ambapo wasichana ni 63,878 na wavulana ni 82,249 sawa na asilimia 33.8 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020,” amesema Ummy.

Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini amesema idadi hiyo ya wanafunzi wenye sifa imejumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalum 288. 

Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 14 kutoka watahiniwa 129,854 waliochaguliwa kujiunga katika ngazi hizo za elimu kwa mwaka 2020.


Zinazohusiana:


Mgawanyo wa kozi

Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano, wanafunzi 41,504 sawa na asilimia 43.4 watajiunga kusoma tahasusi (combination) za sayansi na hisabati.

Hiyo ni sawa kusema katika kila wanafunzi 100 waliopangiwa kuendelea na kidato cha tano 47 watasoma tahasusi za sayansi na hisabati.

“Na wanafunzi 46,159 wakisemo wasichana 24,239 na wavulana 21,920 sawa na asilimia 52 wamechaguliwa kusoma tahasusi za sanaa na biashara,” amesema Waziri Ummy. 

Hivyo wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka 2021 wanapaswa kuanza kuripoti katika shule zao walizopangiwa kuanzia Julai 3 mwaka huu na mwisho wa kuripoti itakua Julai 18, 2021.

“Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine ambaye hatukumpangia katika awamu hii kwanza,” amesema. 

Angalia hapa waliochaguliwa kwenda kidato cha tano 2021 hawa hapa