July 3, 2024

Tanapa yaendelea kuchunguza chanzo cha moto Mlima Kilimanjaro

Yasema jitihada za kudhibiti moto huo zinaendelea huku
taarifa zaidi kuhusu chanzo zinaendelea kufanyiwa kazi.

  • Yasema jitihada za kudhibiti moto huo zinaendelea.
  • Taarifa zaidi kuhusu chanzo zinaendelea kufanyiwa kazi.
  • Yasema shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida. 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) imesema inaendelea kuchunguza chanzo cha kuzuka kwa moto katika Mlima Kilimanjaro huku jitihada za kudhibiti moto huo zikiendelea. 

Moto huo ulizuka Jumapili Oktoba 11, 2020 katika eneo la Whona ambacho ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete katika taarifa yake amesema moto huo unaendelea kudhibitiwa na vikosi vinavyoshiriki zoezi hilo.

Vikosi vinavyoshiriki kuzima moto huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shelutete Oktoba 12, 2020, vinajumuisha wananchi, wanafunzi kwa vitendo na wale wa Mweka (Chuo cha wanyamapori)  na Kikosi cha Zimamoto.

“Taarifa zaidi kuhusu chanzo zinaendelea kufanyiwa kazi,” amesema Shelutete.


Soma zaidi:


Hata hivyo, Tanapa imesema inachukua tahadhari zote ili kuhakikisha usalama wa wageni na vifaa vyao unaimarika bila kuathiri shughuli za utalii ambazo zinaendelea kama kawaida hususan njia ya Marangu iliyoathirika na moto husika.

Mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,340) ni sehemu ya hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 755 na iko umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi mjini. 

 Mlima huo unaopatikana katika mkoa wa Kilimanjaro ni moja kati ya milima ambayo kilele chake hufikiwa kwa urahisi na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapanda milima kutoka kila pande za dunia. 

Mamlaka zinaeleza kuwa wastani wa watu 50,000 hupanda mlima huo kila mwaka.