November 24, 2024

Tanapa yatoa mwongozo wa kurusha ndege zisizo na rubani kwenye hifadhi za wanyama

Mrushaji anatakiwa kupata vibali vinne kikiwemo cha Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA).

  • Mrushaji anatakiwa kupata vibali vinne kikiwemo cha Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA).
  • Mrushaji anatakiwa kufanya maombi rasmi kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa akiambatanisha nakala za vibali.
  • Wakati wa kurusha anatakiwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ikiwemo kurusha ndege umbali usiopungua mita 50 kutoka ardhini. 

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda kupata picha na video nzuri ukiwa katika hifadhi za wanyama kwa kutumia ndege zisizo na rubani, basi una kila sababu ya kujipanga ili kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali.

Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) imetoa mwongozo na taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa kwa  watu wanaorusha ndege zisizo na rubani (Drones) katika maeneo ya hifadhi za Taifa kwa shughuli mbalimbali katika maeneo hayo.

Katika mwongozo uliotolewa na mamlaka hiyo, unaeleza kuwa mtu yeyote hataruhusiwa kurusha ndege hiyo kwenye hifadhi mpaka apate kibali kutoka kwenye mamlaka zinazotambuliwa kisheria. 

Mwombaji anatakiwa apate vibali vinne kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) pamoja na kibali cha Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa.

Hata baada ya kupata vibali hivyo, mhusika anatakiwa kwenda mbali zaidi na  kufanya maombi rasmi kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa akiwa ameambatanisha nakala za vibali kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi, Bodi ya Filamu Tanzania na TCAA.

Mwongozo huo unaeleza kuwa kibali kinabaki kuwa halali pale taratibu zote zinapozingatiwa mhusika anapoanza kutumia ndege hizo akiwa kwenye hifadhi na mamlaka inaweza kuzuia kibali wakati wote kama taratibu vimevunjwa.

Hata hivyo, kwa mtu ambaye atakiuka mwongo na taratibu zilizowekwa za matumizi ya ndege zisizo na rubani kwenye hifadhi anaweza kukabiliwa na dhabu mbalimbali ambazo zimewekwa kisheria. Picha|Mtandao.

Unayotakiwa kuzingatia unaporusha ndege zisizo na rubani kwenye hifadhi

Baada ya kupata vibali na kuruhusiwa kurusha ndege yako ili kujipatia picha na video za matukio mbalimbali, yapo mambo ya msingi unatakiwa kuyafuata ili kuifanya shughuli yako iwe na mafanikio.

Ndege hizo zinatakiwa kurushwa umbali usiopungua mita 50 kutoka kwenye ardhi, hazitakiwi kurushwa kwenye eneo la watalii wengine wasiohusika na mrusha ndege hiyo anatakiwa kutoa taarifa kwa kiongozi wa hifadhi husika kabla hajairusha.

Lakini ndege hizo zinatakiwa kurushwa chini ya uangalizi wa msimamizi wa hifadhi. Kando ya malipo mengine mrusha ndege anatakiwa kulipa gharama ya kurusha na pia  katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ndege hizo hazitakiwi kurushwa wakati wa kuvuka wanyama.

Mwongozo huo unaongeza uzito zaidi kuwa baada ya mrusha ndege kupata picha na video anazozihitaji, anatakiwa kuwasilisha nakala ya alichokipata katika ofisi ya Kamishana wa Uhifadhi kwa ajili ya matumizi yasiyo ya kibiashara. 


Zinazohusiana:


Hata hivyo, kwa mtu ambaye atakiuka mwongo na taratibu zilizowekwa za matumizi ya ndege zisizo na rubani kwenye hifadhi anaweza kukabiliwa na dhabu mbalimbali ambazo zimewekwa kisheria.

“Kukiuka kanuni za hifadhi na masharti yaliyowekwa inaweza kukusababishia kulipa faini ya isiyopungua Sh100,000 au Dola za marekani 100 kwa kosa moja na kutaifisha ndege isiyo na rubani,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo unaopatikana katika tovuti ya Tanapa.