November 24, 2024

Tanzania haitakuwa bora bila kuwashirikisha wanawake kikamilifu

Kuna wanawake wengi wanafanya mazuri lakini kwa sababu mbalimbali mchango wao umekuwa haufahamiki.

  • Kuna wanawake wengi wanafanya mazuri lakini kwa sababu mbalimbali mchango wao umekuwa haufahamiki.
  • Iwapo wanawake watapewa fursa sawa za kimaendeleo, Tanzania itakuwa nchi bora kila nyanja.
  • Nukta tunakuletea mfululizo wa makala za baadhi ya wanawake wanaofanya makubwa katika tasnia mbalimbali. 

Wanawake wamekuwa  kipaumbele katika kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda vizuri kwenye jamii kwa kufanya mambo mengi yanayogusa moja kwa moja maisha yetu. Kila mtu kwa namna moja ama nyingine maisha yake yamekuwa bora zaidi kwa kuwa na mama bora. 

Kina mama hao ndiyo wanaohaha kila siku kutafuta suluhu za maisha kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa. Wengine ni wajasiriamali, madaktari, wakulima, wanasayansi, wapishi, wafanyakazi maofisini, wazalishaji wa maudhui na mambo lukuki. 

Ni hawa hawa wanawake ambao baadhi tunawaita mama, mke, shangazi, dada au binti. Yote wanayofanya yamechangikia Tanzania kuwa hapa. 

Lakini ni wachache wanaofanya makubwa wanatambulika ipasavyo kwa sababu mbalimbali aidha wa kutokuongelewa au kutopewa nafasi zaidi ya kuonekana na kusikilizwa.

Katika  kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka kutambua mchango wa mwanamke, Nukta inakuletea baadhi ya wanawake wanaofanya vizuri katika kada mbalimbali ambao unaweza kuwa umewasikia au hujawahi kuwasikia popote ila wana mchango mkubwa katika kuthubutu kufanya mambo yenye tija katika jamii.

Dhima ya mwaka huu ya “Badili Fikra, Kufika Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu” inahamasisha wanawake kama walivyo wanaume wanapaswa kupewa haki ya kumiliki na kutumia rasilimali ili kujiletea maendeleo.

Licha ya changamoto wanazokutana nazo wanawake wakati wakipigania usawa wa kijinsia, bado wameendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali nchini na kutoa hamasa kwa wasichana wa kike wenye malengo ya kufika mbali katika nyanja zote za maisha zikiwemo za kielimu, biashara  na uongozi.

Katika mfululizo huu wa makala haya hadi Machi 8, 2019 tutakuletea baadhi ya wanawake hawa wa nguvu wakiwemo muongozaji filamu Esther Mndeme  ambaye amekuwa akitumia tasnia hiyo kuleta mabadiliko katika jamii na kujikuza kibiashara na Aneth David, mwanasayansi kijana aliyejikita katika utafiti wa kuongeza tija kwenye kilimo.

Tunaamini kuwa iwapo jamii itatoa fursa sawa kwa wanawake, Tanzania itakuwa nchi bora zaidi itakayokuwa na maendeleo jumuishi katika kila nyanja na itakuwa rahisi kufikia malengo lukuki ya kitaifa kama kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Biashara imara za wanawake zitachangia uchumi kukua na kuajiri wengi jambo litakalopunguza ukosefu wa ajira unaolitafuna Taifa.

Ushiriki kamilifu katika masuala ya sayansi na teknolojia utachochea na kuongeza ugunduzi wa huduma na bidhaa za kisasa kwa kuwa kuna wanawake wabunifu lakini wamekosa fursa ya kuonyesha vipaji vyao.

Tutakuwa tunajidanganya kuwa Tanzania itaendelea bila kubaini uwezo, vipaji na ubunifu walionao wanawake wa nchi hii.

Usikose kufuatilia mfululizo wa makala haya kuanzia Machi 6, 2019.