July 5, 2024

Tanzania ilivyojipanga kuongeza uzalishaji mbegu za kahawa

Itatumia ardhi ya JKT kuzalisha mbegu hizo ili kutosheleza mahitaji ya wakulima.

  • Itatumia ardhi ya JKT kuzalisha mbegu hizo.
  • Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) yatakiwa kuanzisha kitalu cha miche ya kahawa katika kambi ya JKT Kiteule iliyopo ya Tarime. 

Dar es Salaam. Huenda wakulima wa Tanzania wakaongeza uzalishaji na kufaidika zaidi na kilimo cha kahawa baada ya Wizara ya Kilimo kuanza mchakato wa makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kutumia ardhi yake kuzalisha mbegu bora kutosheleza mahitaji ya wakulima.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema kwa kuanzia wizara yake itatoa Sh19 milioni kwa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) ili kuanzisha kitalu cha miche ya kahawa katika kambi ya JKT Kiteule iliyopo ya Tarime mkoani Mara. 

“Wizara ya Kilimo ipo tayari kuingia makubaliano na JKT kuzalisha miche bora mingi ya kahawa ili kutosheleza mahitaji ya wakulima wa mkoa wa Mara na jirani,” amesema Kusaya alipotembelea kambi hiyo mwishoni mwa wiki. 

Akiwa kambini hapo, Kusaya alikagua shamba la kahawa ekari 52 zilizopandwa  kati ya lengo la ekari 200 na kuitaka TACRI kuanza maandalizi ya kufungua kitalu cha miche bora ya kahawa shambani hapo ili wajitosheleze kwa miche na kugawa mingine kwa wakulima.

“Tutahakikisha tunawasaidia JKT ili wakimaliza kupanda ekari zote 200 kahawa taasisi zetu za TFRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea) na zingine zitawezesha upatikanaji wa mbolea na pembejeo ikiwemo mfumo wa umwagiliaji ili shamba hili litumike kama darasa la wakulima wa Tarime kuja kujifunza kilimo bora cha kahawa,” amesisitiza Kusaya.


Soma zaidi:


Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kahawa (2011‐2021) unakusudia kuongeza  uzalishaji wa kahawa hadi kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2021. 

Kambi hiyo ina eneo la eneo la ekari 430 linalofaa kwa kilimo cha kahawa ambapo mkakati wa JKT ni kulima eneo hilo kila mwaka kwa kuongeza ekari 50 na kuwa changamoto iliyopo ni ukosefu wa mfumo wa maji ili kumwagilia kahawa wakati wa kiangazi.

Kusaya amesema watashirikiana na Wizara ya Maji ili kuona namna ya kuweka miundombinu ya maji kwenye shamba hilo kwa kutumia chanzo kilichopo na hatimaye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itafika kuona namna ya kuwa na mfumo wa umwagiliji kwa njia ya matone ili kahawa ikue vema.