July 3, 2024

Tanzania ilivyovuka lengo ukusanyaji mabilioni ya madini 2020-21

Imefanikiwa kukusanya Sh445.2 bilioni ya maduhuli yaliyotokana na vyanzo mbalimbali katika sekta ya madini ikiwemo ada za leseni, jambo ambalo linatia matumaini kwa Watanzania kuendelea kufaidika na sekta hiyo.

  • Imefanikiwa kukusanya Sh445.2 bilioni ya maduhuli yaliyotokana na vyanzo mbalimbali vya madini.
  • Ukusanyaji huo umetokana na kuimarishwa kwa ulinzi wa madini, utoaji wa leseni na kuwabana wadaiwa. 

Dar es Salaam. Serikali imesema imefanikiwa kukusanya Sh445.2 bilioni ya maduhuli yaliyotokana na vyanzo mbalimbali katika sekta ya madini ikiwemo ada za leseni, jambo ambalo linatia matumaini kwa Watanzania kuendelea kufaidika na sekta hiyo.

Ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini umekuwa ukiongezeka mfululizo kila mwaka tangu 2014/15.

Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kiasi hicho cha fedha kimekusanywa katika kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi Machi, 2021. 

Biteko ameliomba Bunge leo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 leo Aprili 29, 2021  kuidhinisha bajeti ya Sh66.8 bilioni katika mwaka ujao wa fedha ambayo imeongezeka imeongezeka kutoka Sh62.7 bilioni zilizotengwa mwaka 2020/21. 

Kati ya fedha hizo za mwaka ujao, Sh15 bilioni (asilimia 22.5) ni fedha za maendeleo.

“…hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya Sh445.2 zimekusanywa na kuwasilishwa hazina ambazo ni sawa na asilimia 112.69 ya lengo la makusanyo la Sh395.1 bilioni katika kipindi husika,” amesema Biteko akibainisha kuvuka kwa lengo lililowekwa awali.


Zinazohusiana:


Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Bukombe amesema maduhuli hayo yametoka na fedha ya ada ya leseni za madini yaliyokuwa Sh18,7 bilioni na ada ya kijiolijia ni Sh5.8 bilioni. 

Maduhuli mengine yametoka kwenye mrabaha wa madini ambapo zilikusanywa Sh357.5 bilioni, adhabu na faini za malimbikizo ya ada (Sh1,8 bilioni) na ada ya ukaguzi wa madini ni Sh61.2 bilioni. 

Ukusanyaji wa mapato hayo umefanikiwa kutokana na Serikali kuweka maafisa migodi wakazi katika migodi mikubwa, ya kati na maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa madini. 

“Vilevile, wizara imeweka wakaguzi wasaidizi wa madini ujenzi kwenye maeneo yenye madini ujenzi na viwandani,” amesema waziri huyo. 

Pia ufuatiliaji wa wadaiwa mbalimbali, kuanzisha na kuendelea kusimamia masoko na vituo vya ununuzi wa madini ambapo hadi Machi, 2021 kuna  masoko 39 na vituo vya ununuzi 50.