Tanzania inavyoweza kufaidika na eneo huru la biashara Afrika
Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania zimetakiwa kuimarisha na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za ndani ili zifaidike kikamilifu na mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA) ikiwemo kupata soko la uhakika la bidhaa.
- Ni kuimarisha na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za ndani ili zifaidike kikamilifu na mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA).
- Pia yatakiwa kuwajengea uwezo wafanyabiashara uwezo wa kutafuta masoko na kutumia teknolojia ya kisasa.
Dar es Salaam. Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania zimetakiwa kuimarisha na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za ndani ili zifaidike kikamilifu na mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA) ikiwemo kupata soko la uhakika la bidhaa.
AfCFTA ni makubaliano ya kibiashara ambayo yanazingatiwa miongoni mwa nchi 27 za Afrika. Ulitiwa sahihi jijini Kigali, Rwanda Machi 21, 2018 ili kuifanya Afrika kuwa eneo kubwa la biashara ulimwenguni.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa 23 wa kamati ya watendaji wa Serikali na wataalamu unaoangazia jinsi ya kusaka fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara wa kikanda kwenye eneo la Mashariki mwa Afrika unaofanyika huko Asmara, Eritrea.
Mkurugenzi wa Utafiti wa kampuni ya Trademark East Africa, Dk Anthony Mveyange aliyekuwa akizungumzia kile ambacho nchi za Afrika zinapaswa kuzingatia ili kunufaika na AfCFTA, amesema nchi za Afrika zinapaswa kufanya biashara kwa ukaribu na kuacha kutegemea bidhaa kutoka nje.
“Eneo ambalo AfCFTA limeonekana kuwa ina nafasi nzuri na chachu ya kuleta maendeleo katika ukanda huu ni kuboresha uwezo wa nchi kuzalisha bidhaa,” amesema Dk Mveyange wakati akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa (UN).
Soma zaidi:
- Mbinu zinazowaweza kuwasaidia wajasiriamali kuchangamkia fursa zilizowazunguka
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Amesema Afrika ina watu takribani bilioni 1.2 ambao ni soko muhimu la bidhaa, jambo linalohitajika ni kuboresha uwezo wa watu kuzalisha ndani ya Afrika na mikakati madhubuti ya kuwezesha nchi kufanya biashara huru.
“Ni namna gani itakuwa rahisi kwa mfano kutoka Ethiopia kufanya biashara na Kenya, badala ya Ethiopia kuagiza bidhaa kutoka China au India, ni namna gani Ethiopia na Kenya zinaweza kufanya biashara kwa urahisi zaidi,” amehoji Dk Mveyange.
Aidha, amesema mikakati yote hiyo inawezekana ikiwa wawekezaji na wafanyabiashara watajengewa uwezo kutumia vizuri masoko na teknolojia ya uzalishaji itakayosaidia kuongeza ajira.
Kampuni ya TradeMark East Africa inashirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Tume ya Uchumi ya umoja huo kwa nchi za Africa (UNECA) na hufanya tafiti pamoja kwa lengo la kuona AcFTA inabadilika kutoka nadharia kuwa vitendo.
Hivi sasa inaendesha shughuli zake Kenya, Zambia, Malawi, Tanzania,Uganda, Rwanda, Ethiopia na wanaelekea Somaliland.