November 24, 2024

Tanzania inavyoweza kunufaika na uwekezaji wa chakula 2020

Hiyo ni baada ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kuainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura wa chakula na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020 ikiwemo Zimbabwe na Sudan Kusini.

  • Hiyo ni baada ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kuainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura wa chakula na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020.
  • Maeneo hayo ni pamoja na Zimbabwe na Sudan Kusini.
  • Tanzania inaweza kutumia fursa hiyo kuuza chakula baada ya mavuno ya 2020. 

Dar es Salaam. Huenda mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania zinaweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa wakulima na kuwawezesha kufaidika na soko katika nchi za Afrika zinazokabiliwa na janga la njaa.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) limeainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura wa chakula na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020 ikiwemo Zimbabwe na Sudan Kusini ambazo zinakabiliwa na mizozo ya kisiasa. 

Kwa mujibu wa ripoti ya WFP ya “Maeneo yaliyoa hatarini duniani 2020” iliyotolewa jana (Januari 2, 2020), inaitaka dunia kuwekeza mabilioni ya fedha mwaka 2020 ili kukomesha hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula inayoongezeka kote duniani.

WFP inakadiria kuwa itahitaji zaidi ya dola bilioni 10 (takriban Sh22.9 trilioni) mwaka huu ili kufadhili operesheni zake katika zaidi ya nchi 80 kote duniani na bila fedha hizo mipango yote ya usaidizi itakuwa njia panda.

“Dunia ni sehemu isiyosameheka na tunapofungua ukurasa mpya 2020, WFP inakabiliwa na changamoto mpya na kubwa zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kuokoa maisha,” inaeleza sehemu ya ripoti ya WFP. 

Maeneo yaliyo na changamoto zaidi ya njaa ni pamoja na nchi ya Haiti inayoshikilia nafasi ya kwanza ikielezewa iko katika hatari kubwa ya kutumbukia zaidi katika mgogoro wa chakula endapo hatua za haraka, msaada na uwekezaji havitopatikana katika miezi ya mwanzo ya mwaka huu. 

“Hatuishi vuzuri, hatuli vizuri na hatuwezi hata kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu ya zahma iliyoikumba nchi yetu,” amesema mmoja wa wakulima wa mbogamboga nchini humo Osena Previlon katika taarifa ya WFP


Zinahusiana: 


Kwa mujibu wa WFP, machafuko ya kisiasa na kijamii yameitumbukiza nchi hiyo katika mtafaruku mkubwa huku bei za chakula zikipanda kwa asilimia 40 na mtu mmoja kati ya watatu nchini humo sawa na watu milioni 3.7 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula vijijini na mijini na miongoni mwao milioni 1 wanakabiliwa na janga la njaa.

Ripoti hiyo imesema Zimbabwe ni nchi nyingine iliyo katika hatari ambayo imeshuhudia ukame mbaya zaidi mwaka 2019 na utakapowadia msimu wa muambo wa Februari, chakula chote kitakuwa kimeisha na watu milioni 7.7 wanakabiliwa na njaa na kuhitaji msaada wa chakula.

Sudan Kusini kwa mujibu wa ripoti hiyo bado kuna mgogoro mkubwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Watu milioni 3.8 wametawanywa na mafuriko ya 2019 ambayo yamewaathiri takriban watu milioni 1 na kuathiri tani zaidi ya 73,000 za nafaka, huku WFP ikibainisha kuwa hali ambayo imewafanya baadhi ya wakulima nchini humo kujiuliza “endapo Mungu amewasahau”

Maeneo mengine yaliyotajwa na ripoti hiyo ni Ukanda wa Sahel, Mali, Burkina Fasso na Magharibi mwa Niger ambako ni kutokana na mchanganyiko wa sababu ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, vita, na mamilioni ya watu kutawanywa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) limeainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura wa chakula na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020 ikiwemo Zimbabwe na Sudan Kusini ambazo zinakabiliwa na mizozo ya kisiasa. .Picha|Henry Be/Unsplash.

Inaweza kuwa fursa kwa Tanzania

Hiyo inaweza ikawa fursa kwa wakulima wa Tanzania kufaidika na uwekezaji ambao WFP inatarajia kuufanya kuzisaidia nchi zenye ukosefu wa chakula kwa kuuza mazao yao hasa mahindi ambayo husafirishwa hadi katika maeneo yenye migogoro. 

Mwishoni mwa mwaka 2019, Tanzania iliuzia Zimbabwe tani 7,000 za mahindi ikiwa ni muendelezo nchi hiyo kukabiliana na upungufu wa tani 800,000 za mahindi kwa watu wake. 

Septemba 3, 2019, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi wakati anatoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba leo, alisema shughuli za kawaida za kilimo zitaenda vizuri kwa sababu mvua zitakuwepo za kutosha.

Kutokana na kuwepo kwa mvua za kutosha, wakulima wanaweza wakapata mavuno mazuri mwaka 2020, jambo linaloweza kufungua fursa za kufaidika na kilimo hicho hasa katika nchi za Afrika.