November 24, 2024

Tanzania inavyoweza kupunguza vifo vya watoto vinavyotokana na ajali za barabarani

Ni kwa kutoa elimu na kujenga miundombinu rafiki kwa watoto ikiwemo njia za watembea kwa miguu karibu na shule ili kuwakinga na ajali ambazo zimekuwa zikikatisha ndoto zao.

  • Ajali za barabarani ni miongoni mwa visababishi vikubwa vya majeraha na vifo kwa watoto.
  • Ajali hizo hutokea kwa sababu ya kutukuwepo miundombinu rafiki kuwakinga watoto.
  • Wadau, Serikali wasisitiza kufuatwa kwa sheria na programu za kuwalinda watoto.

Geita. “Tunapata shida sana tunapovuka barabara kuingia shuleni maana gari zinapita kwa kasi sana hapa,” anasema Happiness Shelembi, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita. 

Happiness (17) anasoma katika shule hiyo iliyopo mita chache kutoka barabara kuu ya Kahama-Bukoba katika eneo la shule. Katika eneo hilo, hakuna miundombinu rafiki inayoweza kuwahakikishia usalama wao wanapoingia shuleni.

“Wakati wa kuvuka inabidi tujikusanye makundi ili madereva wakituona wapunguze mwendo,” anasema msichana huyo anayesoma kidato cha nne shuleni hapo.Wanafunzi wa shule hiyo hukumbana na ajali za magari na pikipiki na kuwasababishia majeraha mwilini.

Happiness ni miongoni mwa wanafunzi wengi Tanzania na duniani wanaohatarisha maisha na ndoto za elimu kutokana kucheza, kuishi na kusoma katika shule zilizo karibu na barabara.

Hali hiyo huwafanya wapate ajali wakati wa kutembea kwa miguu, kuendesha baisketi na vyombo moto hasa pikipiki kutoka na changamoto mbalimbali za barabarani ikiwemo ukosefu wa miundominu rafiki.

Pia kuongezeka kwa magari, kutozingatia kwa sheria za usalama barabarani ikiwemo mwendo kasi, ulevi navyo vinaongeza hatari  ya watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupata ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa ripoti ya “athari za ajali za barabarani kwa watoto” iliyotolewa na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) na taasisi ya Abertis mwaka 2019 inaeleza kuwa asilimia 22 ya vifo vya watoto duniani vinatokana na majeraha yanayosababishwa na ajali za barabarani.

Nalo Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa watoto wa kiume ndiyo wako katika hatari zaidi kupata ajali za barabarani ambapo asilimia 73 ya vifo vya barabarani kwa watoto huwapata wavulana huku zaidi ya asilimia 90 ya ajali zote duniani hutokea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Ajali za barabarani siyo tu zinakatisha maisha ya wanafunzi, kuwaachia majeraha na kuathiri elimu yao, bali huchangia kuathiri uchumi wa wazazi, familia na Taifa kutoka na kutumia gharama kubwa  zao matibabu, kuwalea walemavu na kupoteza nguvukazi kwa ajili ya maendeleo.

Licha ya kuwa kuna kazi kubwa imefanyika na Serikali na wadau wa maendeleo kupunguza ajali za barabarani, juhudi zinahitajika zaidi kuwalinda watoto hasa katika maeneo ya shule ambayo yako karibu na barabara zenye muingiliano mkubwa wa magari na watu.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG’s) ya mwaka 2030 yanazitaka nchi ikiwemo Tanzania kuhakikisha zinatoa mifumo ya usafiri iliyo salama yenye uhakika na kuboresha usalama barabarani kwa watu wote huku msisitizo ukitakiwa kuwekwa kwa makundi ambayo yako katika hatari ya kuathirika zaidi wakiwemo watoto.

Hatua zinazochukuliwa

Mkuu wa Shule ya Masumbwe, Yusuph Maguma anasema wanashirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha usalama wa wanafunzi wawapo shuleni ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuboresha miundombinu ili kuwalinda na hatari zozote ikiwemo ajali.

“Kazi inafanyika tunatoa elimu kwa wanafunzi kutumia barabara vizuri hasa wanapokuja na kutoka shuleni kuwakinga na madhara yanoyoweza kuwapata,” anasema Maguma.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Boniface Singu wa kidato cha nne anasema wanatumia elimu wanayopata ya usalama barabarani kuepuka changamoto za barabarani lakini wangependa wahakikishiwe usalama wao zaidi. 


Suluhu ya kudumu ya ajali za barabarani kwa watoto

Kwa mujibu, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto Duniani katika andiko la la “namna ya kuwalinda watoto”, wanaeleza kuwa jamii inapaswa kuwaelimisha watoto kwa usahihi matumizi ya barabara ikiwemo wanaotembea kwa miguu na wale wanaotumia vyombo vya moto.

“Hakikisha watoto wanavaa kofia ngumu wakati wanaendesha pikipiki au baiskeli,” imeeleza sehemu ya andiko hilo huku akibainisha kuwa watoto washauriwe kuvaa nguo nyeupe au zinazoakisi mwanga kila wanapovuka barabara  hasa maeneo ya shuleni ili iwe rahisi kwa madereva wa vyombo vya moto kuwaona.

Miundombinu hiyo ni pamoja na kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakuwa na sehemu ya wapita kwa miguu ambayo ina vizuia ambavyo vinaweza kumkinga mtoto asifikiwe kirahisi na vyombo vya moto. Picha| Amend Tanzania.

Balozi wa usalama barabarani (RSA), Ramadhan Msangi anasema kuna haja ya kuzifanyia maboresho sera na sheria zinazosimamia usalama barabarani ili kulipa kipaumbele kundi la watoto kwa sababu limekuwa likiathirika zaidi na ajali ambazo zinaweza kuzuilika. 

“Vyombo vya maamuzi navyo vilione jambo hili kuwa lina muhimu hasa pale wanapoandaa sheria, sera na miongozo mbalimbali kuhusu matumizi ya barabara. Na ziwekwe adhabu kubwa kwa watu ambao wataonyesha kukiuka sheria au taratibu zinazohusiana na usalama wa watoto barabarani,” anasema Msangi.

Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ndiyo inayosimamia watumiaji wa barabara Tanzania  ili kufanya matumizi ya barabara kuwa ya tija na manufaa. 

Pia imewekwa kuepusha makosa ambayo yatasababisha hasara ya miundombinu na hasara juu ya maisha ya watu na mali zao wanapotumia barabara.

Wakati wadau wakitaka elimu itolewe na sheria na kanuni za barabarani zizingatiwe, wadau wengine wamependekeza programu maalum ya tathmini na uboreshaji wa maeneo ya shule yaliyopo karibu na barabara (SARSAI). 

Programu hiyo ambayo ilifanyiwa utafiti na taasisi ya Amend Tanzania na Kituo cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa cha Marekani (CDC) jijini Dar es Salaam imeonyesha matokeo mazuri kwa sababu inapunguza kwa asilimia 40 ajali za barabarani zinawakumba watoto hasa katika miji inayokua kwa haraka Afrika.


TANGAZO:


Mkurugenzi Mkaazi wa Amend Tanzania, Simon Kalolo anasema mapendekezo ya programu hiyo ambayo imehakikiwa kisayansi ni kujenga miundombinu rafiki na salama katika maeneo ya shule ambayo yatawakinga wanafunzi wanapotumia barabara. 

Miundombinu hiyo ni pamoja na kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakuwa na sehemu ya wapita kwa miguu ambayo ina vizuia ambavyo vinaweza kumkinga mtoto asifikiwe kirahisi na vyombo vya moto.

Pia uwepo wa alama za pundamilia ambazo watembea kwa miguu wanakatiza barabara na waendesha vyombo vya moto waelimishwe kuheshimu.

Sambamba na hilo, Kalolo anasema maeneo ya shule yajengewe matuta na vibao maalum vilivyo na alama mbalimbali ikiwemo ya wavuka kwa miguu, kupunguza mwendo ili kuwadhibiti madereva wasumbufu.

“Tunatumia fursa mbalimbali kushawishi usanifu wa barabara uzingatie mahitaji na usalama watoto na watumiaji wengine. Pia tunahisii Serikali itekeleze sera na viwango vya miundombinu salama kwa watumiaji wote wa barabara,” anasema Kalolo. 

Serikali yasisitiza kufuata sheria

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene katika hotuba ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 aliyowasilisha hivi karibuni bungeni, anasema Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu kwa umma, kuchukua hatua kali kwa wanaokiuka sheria.

Pia kuanzisha kanzidata ya kuwatambua madereva wa bodaboda na hivyo kuongeza ufanisi katika usimamizi wa usalama barabarani.

“Ninatoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuendelea kutii sheria za barabarani ili kuhakikisha usalama wao,” anasisitiza Simbachawene.