October 7, 2024

Tanzania kukopa takriban Sh8 trilioni bajeti 2020-21

Fedha hizo ni kati ya Sh33.88 trilioni ambazo Serikali inatarajia kukusanya katika bajeti hiyo kutoka katika vyanzo mbalimbali vya ndani na nje.

  • Fedha hizo ni kati ya Sh34.88 trilioni ambazo Serikali inatarajia kukusanya katika bajeti hiyo.
  • Kiasi cha Sh10.48 trilioni kitatumika kulipia deni la Serikali.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepanga kukusanya na kutumia Sh34.88 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2020/21 huku ikitarajia kukopa Sh7.94 trilioni kutoka kwenye masoko ya fedha ya ndani na nje kugharamia mahitaji ya bajeti hiyo ya mwisho ya kipindi cha kwanza cha Serikali ya Rais John Magufuli.

“Serikali inatarajia kukopa Sh4.9 trilioni kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 3.32 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Shilingi trilioni 1.59 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo,” Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ameliambia Bunge Jumanne wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali.

Dk Mpango amesema mbali na kiwango hicho kitakachokopwa soko la ndani, Sh 3.04 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Katika bajeti hiyo, wahisani wa maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu jumla ya Sh2.87 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 8.2 ya bajeti.


Zinafanana:


“Kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo ni shilingi trilioni 2.46; mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 138.3; na misaada na mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) Sh 275.5 bilioni,” amesema waziri huyo jijini Dodoma.

Mbali na mikopo na fedha za wahisani, Serikali hiyo inayotekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa na ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la Mwalimu Nyerere la Megawati 2,100, inatarajia kukusanya mapato ya kodi Sh20.33 trilioni mwaka 2020/21 kutoka Sh19.1 trilioni katika mwaka unaoishia Juni 30.

Mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh2.92 trilioni wakati mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Sh815 bilioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh765.5 bilioni zilizotarajiwa katika mwaka 2019/20.

Katika mwaka huo wa fedha unaoanza Julai Mosi, Dk Mpango amesema kati ya Sh22.1 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh10.48 trilioni zitatumika kulipia deni la Serikali huku Sh7.76 trilioni kwa ajil ya mishahara ya watumishi wa umma.

Tofauti na bajeti za miaka iliyopita, bajeti hii pia imeangazia kutoa nafuu kwa wazalishaji na watumiaji kutokana na kutoongeza ushuru maalumu kwa bidhaa zisizo za petrol kutokana na kuwa biashara nyingi zimeshaathirika na COVID-19.