October 6, 2024

Tanzania kunufaika na mabilioni ya FAO

Mfuko huo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO) umetengewa dola za Marekani 174 milioni (Sh402.6 bilioni) kwa ajili ya miradi 24 ya kilimo na mazingira katika nchi 30 duniani.

  • Ni miongoni mwa nchi 30 duniani zitakazofaidika na mfuko wa mazingira duniani (GEF). 
  • FAO imetenga Sh402.6 bilioni kwa ajili ya miradi 24 ya kilimo na mazingira. 
  • Tanzania itasaidia kuboresha udongo katika maeneo yenye migogoro ya ardhi. 

Dar es Salaam. Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zitakazofaidika na mfuko wa mazingira (GEF) unaoshughulikia changamoto za kilimo na mazingira ili kuhakikisha dunia inakuwa na mifumo endelevu ya upatikanaji wa chakula.

Mfuko huo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO) umetengewa dola za Marekani 174 milioni (Sh402.6 bilioni) kwa ajili ya miradi 24 ya kilimo na mazingira katika nchi 30 duniani.

Taarifa ya FAO iliyotolewa mjini Roma, Italia imesema kuwa hatua hiyo imetangazwa wakati wa mkutano wa 58 wa GEF uliofanyika kwa njia ya mtandao, ikiwa ni mara ya kwanza kutokana na janga la Corona au COVID-19.

Miradi hiyo inajikita kwenye madhara ya majanga ya mazingira katika kilimo ambapo miradi minne katika nchi za  Nicaragua, Guinea, Kenya na Uzbekistan itachangia katika kuimarisha mifumo ya chakula, matumizi na uhifadhi wa ardhi. 

Katika mradi wa nchini Tanzania, ulioanzishwa mwaka 2019 kinachofanyika ni kushughulikia mmomonyoko wa udongo na mifumo anuai katika ardhi zenye ukame ili kuongeza rutuba kwa ajili ya kilimo. 

Mradi huo unatekelezwa katika Wilaya za Mvomero, Malinyi, Kilosa na Ulanga mkoni Morogoro ambako kuna changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji kuhusu matumizi ya ardhi. 

Mfuko huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia unalenga kutunza bayoanuai kwa kujumuisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa mapana zaidi.


Zinazohusiana:


Katika miradi mingine minne, FAO itaweza kusaidia nchi tisa zisizo na bahari, visiwa vidogo na zinazoendelea kukabiliana na hatari za kipekee za mazingira katika maeneo yao.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu amesema miradi hiyo iliyopitishwa imebuniwa kwa lengo la kuimarisha mifumo ya chakula ya kitaifa huku ikizingatia uhifadhi wa mazingira kwa maslahi ya binadamu na sayari dunia. 

“Hii itasaidia wakulima, wavuvi, na waendelezaji wadogo wa misitu ili kupanua wigo wa njia zao za kujipatia kipato na kuongeza pia udhibiti kwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19,” amesema Dongyu.

FAO iliyoanza kuwa wakala wa GEF mwaka 2006 imeshasaidia zaidi ya serikali 130 na kutekeleza zaidi ya miradi 200 yenye thamani ya mabilioni ya dola ambayo hadi sasa imenufaisha takribani wanawake na wanaume wapatao milioni 5.