October 6, 2024

Tanzania kutekeleza masharti mkopo wa elimu Benki ya Dunia

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali itatekeleza kikamilifu masharti ya mkopo wa dola za Marekani 500 milioni uliotolewa na Benki ya Dunia ikiwemo kuwawezesha wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kuendelea n

  • Waziri wa Elimu Prof Joyce Ndalichako amesema watatekeleza masharti yote ya mkopo huo.
  • Amesema hawatawabagua wasichana waliopata mimba bali wataruhusu kuendelea na masomo. 
  • Mkopo huo wa Sh1.2 trilioni unakusudia kuongeza ubora wa elimu ya sekondari nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali itatekeleza kikamilifu masharti ya mkopo wa dola za Marekani 500 milioni uliotolewa na Benki ya Dunia ikiwemo kuwawezesha wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo. 

Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na mjadala mpana katika mitandao ya kijamii kuhusu masharti ya mkopo huo ambapo msichana aliyepata mimba atakuwa na hiari ya kuendelea na masomo katika mfumo rasmi au katika elimu nyingine ikiwemo ya kukuza ujuzi na ufundi stadi.

Prof. Ndalichako katika taarifa yake iliyotolewa jana (Aprili 6, 2020) amesema watatekeleza mkopo huo ambao utakuwa chini ya mradi wa uboresha wa elimu ya sekondari (SEQUIP). Mradi huo utawafaidisha takriban wanafunzi milioni 6.5 wa shule za sekondari wakiwemo wasichana waliopata mimba bila ubaguzi

“Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa (wasichana waliopata mimba ) wanaendelea na masomo kama ilivyoelezwa kwenye mradi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Amesema wanafunzi wote watakaofanya mitihani ya Taifa watapata fursa sawa ya kuendelea na masomo katika shule za umma, vyuo, vyuo vikuu bila kujali taasisi za elimu walizotoka. 

Waziri huyo amewahakikishia wabia kuwa Serikali itatekeleza kikamilifu mradi huo kama walivyokubaliana lengo ikiwa ni kuboresha elimu ya wanafunzi wa Tanzania.


Zinazohusiana: 


Aidha, amesema watashirikiana na wadau zikiwemo Asasi za Kiraia (Azaki) katika kila hatua ya mradi huo ambao utakuwa unatolewa kwa awamu kulingana na utekelezaji wa majukumu yaliyoanishwa. 

Awamu ya kwanza ya mkopo huo itaanza kutolewa mwaka 2021.

Mkopo huo wa Sh1.2 trilioni unakusudia kuongeza ubora wa elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa, maabara, mabweni na nyumba za watumishi na vifaa vya kufundishia. 

Benki hiyo iliidhinisha mkopo huo Machi 31, 2020 na kueleza kuwa utasaidia watoto wa Tanzania kupata elimu na kumaliza elimu ya sekondari katika mazingira salama na bora ya kujifunzia. 

Hata hivyo, Benki ya Dunia imeahirisha kupitisha mkopo huo muhimu mara kadhaa kutokana na kutoridhishwa kwake na sera ya Serikali kuwazuia wanafunzi wajawazito kwenda shule.