November 24, 2024

Tanzania kutumia ndege za kukodi kusafirisha mazao ya bustani nje ya nchi

Serikali imesema wakati ikisubiri kukamilika kwa mchakato wa ununuzi wa ndege ya kubeba mazao ya bustani, inaangalia uwezekano wa kutumia ndege za kukodi kufanikisha biashara hiyo ya usafarishaji wa mazao hayo nje ya nchi.

  • Imesema itatumia ndege hizo za kukodi wakati ikisubiri kukamilika kwa ununuzi wa ndege zake.
  • Ndege hizo zitakuwa zinatumia viwanja vya ndege vya Mwanza na Songwe mkoani Mbeya.

Dar es Salaam. Serikali imesema wakati ikisubiri kukamilika kwa mchakato wa ununuzi wa ndege ya kubeba mazao ya bustani, inaangalia uwezekano wa kutumia ndege za kukodi kufanikisha biashara hiyo ya usafarishaji wa mazao hayo nje ya nchi. 

Mazao ya bustani (horticulture crops) ambayo hujumuisha mboga mboga, maua na matunda yamekuwa yakihitajika sana katika nchi zilizoendelea ikiwemo Ulaya. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliyekuwa akizungumza leo (Novemba 13, 2019) bungeni jijini Dodoma amesema mchakato wa ununuzi wa ndege ya kubeba mazao hayo tayari umeanza. 

“Tayari tuna miezi mitatu tulishaanza kujadiliana jinsi ya kupata ndege ya kubeba hortculture kutoka kiwanja cha ndege cha Songwe lakini pamoja na minofu ya samaki kutoka Mwanza,” amesema Mhandisi Kamwelwe. 

Amesema wakati wakisubiri kukamilika kwa mchakato huo, watatumia ndege za kukodi ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kufaidika kikamilifu na biashara ya mazao hayo nje ya nchi. 


Soma zaidi:


Waziri huyo amebainisha kuwa shirika la ndege la KLM la Ufaransa lina ndege moja ambayo inatoa huduma ya kusafirisha mazao hayo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na changamoto imebaki katika mikoa ya Mbeya na Mwanza ambayo ina rasilimali hizo. 

“Kwahiyo tutaanza kwanza na kukodi ndege, kwa sababu kuna changamoto ya kubeba mizigo kutoka Ulaya kuleta huku lakini kutoka hapa kwenda kule mzigo upo. 

“Kwanza tunaanza na kukodi, baadaye tunaweza tukanunua,” amesema Waziri Kamwelwe wakati akijibu swali la Mbunge wa Rombo (Chadema) Joseph Selasini  aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kununua ndege ya mizigo hasa kwa ajili  ya mazao ya bustani. 

Katika swali lake, Selasini amesema mikoa ya kaskazini mwa Tanzania ina eneo zuri kwa ajili ya kilimo cha mazao ya bustani na bado wakulima hawajafaidika. 

“Kwanini mkakati wa hortculture authority (Mamlaka ya mazao ya bustani), mkakati wa kutafuta masoko, tusiangalie kama nchi kununua ndege ya mizigo maana yake mazao haya ya hortculture yanakwenda Nairobi yanasafirishwa kwa ndege za Kenya,” amehoji Selasini.