Tanzania yaanza mazungumzo na wawekezaji bandari ya Bagamoyo
Rais Samia Suluhu Hassan aeleza kuwa Serikali imeanza mazungumzo na wawekezaji wa mradi huo ili uendelee na kuleta faida kwa taifa.
- Rais Samia Suluhu Hassan aeleza kuwa Serikali imeanza mazungumzo na wawekezaji wa mradi huo ili uendelee na kuleta faida kwa taifa.
Dar es Salaam. Baada ya kukwama kwa muda mrefu, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali imeanza kufanya mazungumzo na wawekezaji wa mradi wa bandari ya Bagamoyo utakaogharimu Dola za Marekani 10 bilioni zaidi ya Sh23 trilioni.
Mradi huo wa bandari ya Bagamoyo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya matrilioni nchini iliyokuwa imekwama kutokana na kutokamilika kwa majadiliano ya kiuwekezaji baina ya Serikali na wawekezaji ukiwemo wa mradi mtambo wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas) uliopo mkoani Lindi wenye thamani ya Dola za Marekani 30 bilioni au zaidi ya Sh70 trilioni.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC), Rais Samia amedokeza kuwa tayari Serikali imeanza mazungumzo na wawekezaji wa mradi huo wa Bagamoyo.
“Naomba niwape taarifa njema kuwa tumeanza mazungumzo ya kufufua mradi wote wa Bagamoyo pamoja na Mchuchuma na Liganga,” amesema kiongozi huyo wa juu leo Juni 26 jijini Dar es Salaam.
“Bagamoyo nayo tunakwenda kuanza mazungumzo na ile taasisi (mwekezaji) iliyokuja kwa ajili mradi huo ili nao tuufungue tuende nao kwa faida yetu na kwa ajili ya faida ya wawekezaji,” amesema.
Tangu aingie madarakani Rais Samia amekuwa akisisitiza kuboresha mazingira ya biashara na kusisitiza ufufuaji wa majadiliano na wawekezaji wa miradi mikubwa nchini ukiwemo huo wa LNG.
Mradi wa Bagamoyo utahusisha ujenzi wa bandari na eneo la uwekezaji na kuifanya kuwa bandari kubwa zaidi Afrika Mashariki zaidi ile ya Mombasa.
Wawekezaji wa mradi huo China Merchants Holding International kutoka China na State General Reserve ya Oman walishakuwa wameanza kufanya majadiliano na kusaini mkataba na Serikali tangu mwaka 2013.
Juni 2019 hayati Rais John Magufuli alieleza kuwa wawekezaji hao walileta masharti ambayo ni magumu katika utekelezaji wake.