July 8, 2024

Tanzania yaombwa kushughulikia adha za madereva kwenye mipaka

Chama cha wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) kimeiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi changamoto nne ikiwemo unyanyasaji wa madereva wa Tanzania katika mpaka wa nchi za Rwanda na Kenya.

  • Changamoto hizo ni kuzuiawa kuingia katika nchi za Rwanda na Kenya wakati huu wa janga la Corona.
  • Walalamika kunyanyaswa na kutopata huduma za kijamii katika mipaka hiyo.
  • Wasema hali hiyo inawaletea hasara katika biashara zao. 

Dar es Salaam. Chama cha wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) kimeiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi changamoto nne ikiwemo unyanyasaji wa madereva wa Tanzania katika mpaka wa nchi za Rwanda na Kenya ili kuimarisha shughuli za kibiashara katika nchi hizo.

Changamoto hizo zimeibuka wakati huu wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.

Mwenyekiti wa TATOA, Angelina Ngalula katika taarifa yake iliyotolewa (Juni 8, 2020) amesema madereva wa malori wa Tanzania wamekuwa wakinyanyaswa na kunyanyapaliwa wanapotaka kuingia katika nchi za Kenya na Uganda.

“Wapo madereva ambao wamekaa muda mrefu katika mpaka wa Rusumo wakisubiri kushusha mzigo na wengine wakisubiri kuvuka kwenda nchini Congo,.

“Madereva hawa wamekuwepo katika eneo ambalo halina huduma toshelezi za kijamii kwa idadi kubwa ya madereva wanaosubiri kuvuka,” amesema Ngalula. 

Ngalula amesema kwa utaratibu uliopo sasa gari za Tanzania zinatakiwa kuishia mpakani isipokuwa kwa zile zilizobeba mizigo iliyoainishwa kama bidhaa muhimu.

Wakati huo huo gari za Rwanda zinaruhusiwa kusafiri zaidi ya kilomita1,000 kuja Dar es Salaam kuchukua mizigo bila bugudha yoyote na kupeleka mizigo hiyo hadi mlangoni kwa wateja.

Amesema hali hiyo inasababisha kutokuwepo kwa usawa wa ufanyaji biashara baina ya nchi hizi mbili. 


Zinazohusiana: 


Mbali na changamoto hiyo, Ngalula amesema gharama za ufanyaji biashara katika mpaka wa Rusumo mkoani Kagera zimeongezeka kwani eneo lililotengwa na serikali ya Rwanda lina miundombinu hafifu ya ushushaji mizigo. 

“Ucheleweshaji huu unasababisha wasafirishaji wa Tanzania kuendelea kutozwa faini za makontena ya hadi Sh120,000 kwa siku kwa kontena moja.

“Wanachama wa TATOA wako katika wakati mugumu unaoweza kupelekea kufilisika kutokana na gharama za tozo zinazosababishwa na ucheleweshaji katika mpaka wa Rwanda,” amesema Ngalula.

Changamoto nyingine ni kutokuzingatiwa kwa vyeti vinavyoonyesha kuwa mtu amepimwa Covid-19 ambapo makubaliano ni kuwa dereva mwenye cheti hicho anaruhusiwa kupita mpakani bila vikwazo.

“Kuvikataa vyeti hivyo tena bila taarifa kunasababisha madereva kuendelea kupata tabu katika mpaka wa Namanga na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara hasa waosafirisha bidhaa zinazoharibika kwa haraka (perishable),” amesema Ngalula.

TATOA imeiomba Serikali kuzitazama changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi ili nchi ifaidike kwa mapato na wao waendelea kufanya biashara kama ilivyo kuwa awali.