November 24, 2024

Tanzania yapata heshima ya kushiriki maonyesho ya biashara China

Yaalikwa kama mshirika maalum kutoka Afrika katika maonyesho hayo yanayofanyika kwa mara ya 15 nchini China.

  • Yaalikwa kama mshirika maalum kutoka Afrika katika maonyesho hayo yanayofanyika kwa mara ya 15 nchini China.
  • Ni uwanja wa Tanzania kujitangaza katika sekta za biashara, utalii na teknolojia.
  • Makamu wa Pili wa Rais wa Zazibar, Balozi Seif Ally Idd kuiwakilisha Tanzania akiungana na viongozi wa Serikali na wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Kuna kila dalili kuwa wafanyabiashara wa Tanzania wataendelea kufaidika na fursa za masoko ya bidhaa katika nchi zilizoendelea baada ya Serikali kuimarisha mafungamano ya kibiashara na nchi ya China.

Safari hii Tanzania inatarajiwa kuwa mshiriki maalum katika maonyesho ya 15 ya biashara yanayohusisha China na nchi za Mashariki mwa bara la Asia (CHINA-ASEAN EXPO) yatakayofanyika katika Jiji la Nanning, China.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Biashara na Viwanda ya China, maonyesho hayo yatafanyika kuanza Septemba 12 hadi 15, 2018, Tanzania itakuwa mshirika maalum kutoka Afrika kushiriki jukwaa hilo muhimu la maonyesho ambalo linalenga kuwakutanisha watu mbalimbali duniani kubadilishana uzoefu na fursa za kibiashara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ally Iddi ataiwakilisha nchi akiongozana na jopo la viongozi wa Serikali pamoja na wafanyabiashra mbalimbali.

Maonyesho hayo yatahusisha shughuli mbalimbali ambapo Tanzania itanufaika katika kujitengenezea fursa ya kukutana na wawekezaji na kujitangaza zaidi katika sekta ya utalii na biashara.

Ukumbi wa Maonyesho wa Kimataifa maarufu kama viwanja vya Sabasaba ambapo ni makutano ya wafanyabiashara wengi nchi Tanzania kipindi cha mwanzoni mwa mwezi Julai kila mwaka.Picha| parstoday.com

Pia itakuwa ni fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuonyesha bidhaa zao hasa za kilimo na zile zinazotengenezwa kwa mkono ambapo zitapata fursa ya kunadiwa na zaidi ya vyombo 170 duniani.

Ushirikiano wa China na Tanzania kibiashara kwa mwaka 2017 ulifikia Dola za Marekani bilioni 3.4 (Sh 7.7 trilioni), hivyo kwa Tanzania kushiriki maonyesho haya itakuwa ni fursa adhimu kuvutia wawekezaji wengii kutoka nchi za Mashariki mwa bara la Asia kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.


Zinazohusiana: Tanzania kunufaika mkataba wa uhifadhi malikale, utamaduni


Hata hivyo ushirikiano huu ni moja ya njia za kuongeza mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizi mbili huku China ikijikita zaidi katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika sekta ya kilimo, utalii, afya, miundombinu na biashara.

Septemba 3, 2018, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alishiriki katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano Kati za Afrika na China Kwenye ukumbi wa Mikutano wa Great Hall of the People uliopo Beijing uliowakutanisha viongozi wa Afrika kujadili ushirikiana na nchi katika sekta mbalimbali.

Mtaalam wa masuala ya uchumi Prof. Honest Ngowi, kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi la Dar es Salaam amesema hii ni fursa nzuri kufahamiana na kampuni mbalimbali na kujitangaza kiuchumi.

“Uwezekano wa kuunganishwa na wawekezaji ni mkubwa kutokana na kuwa na nchi nyingi na wafanyabiashara mbalimbali katika eneo moja,” amesema Ngowi.

Amebainisha kuwa itakuwa ni fursa muhimu ya kuunganishwa katika masoko makubwa ya kimataifa ambayo yanahitaji biadhaa kutoka Tanzania hasa za kilimo na kuwafaidisha watanzania wengi.