July 3, 2024

Tanzania yapokea dozi milioni 1 za chanjo dhidi ya COVID-19

Chanjo hiyo ni msaada kupitia mpango wa usambazaji chanjo kwa nchi zenye uchumi wa chini wa Covax.

  • Chanjo hiyo ni msaada kupitia mpango wa usambazaji chanjo kwa chini ya uchumi wa chini wa Covax. 
  • Balozi wa Marekani nchini Tanzania amesema ugawaji huo umelenga kuokoa maisha ya watu na kudumisha mshikamano na Tanzania na Marekani.

Dar es Salaam. Tanzania imepokea dozi zaidi ya milioni moja za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) iitwayo Johnson & Johnson ikiwa ni msaada kupitia mpango wa usambazaji chanjo wa Covax ulioratibiwa na Umoja wa Afrika (AU).

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright amesema wametoa chanjo hizo ili kuokoa maisha ya watu lakini pia kuendeleza mshikamano na Tanzania.

“Tunatoa chanjo hizi kuokoa maisha ya watu na kulimaliza janga hili duniani. Utoaji wa chanjo hizi utakua kielelezo cha mshikamano wa miaka 60 na nchi ya Tanzania,” amesema Wright.Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright akikabidhi chanjo katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Picha| Ubalozi wa Marekani Tanzania.

Chanjo hizo, zilizopokelewa leo mchana (Julai 24, 2021) katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),  ni sehemu ya mpango wa nchi ya Marekani kugawana na nchi mbalimbali duniani kama moja ya jitihada za kupambana na ugonjwa wa Corona duniani.

Mapokezi hayo yamefuatia maamuzi yaliyotolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Juni 28, 2021 kuwa Tanzania iliomba kujiunga na mpango wa Umoja wa Mataifa wa upatikanaji wa chanjo wa COVAX kwa nchi za kipato cha chini. 

Jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Dorothy Gwajima aliwaambia wanahabari Dar es Salaam kuwa mpango wa Serikali ni kutoa chanjo asilimia 60 ya watu wote nchini.