Tanzania yapokea ndege ya tano aina ya De Havilland
Rais Samia Suluhu Hassan amewaongoza viongozi na wananchi kuipokea ndege aina ya De Havilland kutoka Canada ambapo sasa Serikali itakuwa na ndege tano za masafa mafupi.
- Ni ndege ya tano ya masafa mafupi iliyonunuliwa na Serikali.
- Rais Samia aagiza ndege hiyo zitunzwe ili ilete manufaa.
- Itasaidia kufungua fursa za biashara, utalii na ajira kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaongoza viongozi na wananchi kuipokea ndege aina ya Bombardier Dash 8-Q400 (De Havilland (DHC)) ambayo Serikali imeinunua na kufanya Tanzania kuwa na ndege tano za masafa mafupi.
Ndege hizo tano ni miongoni mwa ndege tisa ambazo Serikali imezinunua katika awamu ya tano na sita.
Baadhi ya viongozi waliokuwepo wakati wa mapokezi hayo ni Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege iliyowasili kutoka Canada katika katika uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam amesema ndege hiyo itasaidia kufungua fursa mbalimbali biashara, utalii na kutoa ajira kwa Watanzania.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi ameagiza ndege zote zilizonunuliwa na Serikali ikiwemo iliyowasili leo zitunze ili zilete manufaa kwa Taifa na hujuma zote zidhibitiwe.
“Ndege hizi tumezipata kwa jasho na damu nataka niwaombe sana watumishi wa shirika kuwa makini katika utumiaji na uhudumiaji wa ndege hizi tunazozinunua,” amesema Rais Samia muda mfupi kabla ndege hiyo haijatua uwanjani.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuliimarisha Shirika la ndege Tanzania (ATCL) ili lijiendeshe kwa ufanisi na faida ambapo tayari amepokea mpango kazi wa kibiashara wa uendeshaji shirika hilo kwa ajili ya uhakiki.
Baada ya ndege hiyo kupokelewa imekabidhiwa kwa Shirika la ndege Tanzania (ATCL) kwa ajili ya uendeshaji ambapo Mtendaji Mkuu ATCL, Ladislaus Matindi amesema ni miongoni mwa ndege tano za masafa mafupi ambazo zinamilikiwa na Serikali.
Ndege hiyo iliyowasili leo jioni Julai 30, 2021 ni sehemu ya ndege tatu ambazo Serikali ilishakamilisha malipo ya ununuzi tangu mwezi Aprili.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia wabunge jijini Dodoma Aprili 13, 2021 kuwa kati ya ndege hizo tatu, mbili ni Airbus A220-300 wakati iliyosalia ambayo imewasili leo ikiwa ni De Havilland.
“Ndege hizo zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/22 na hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na ndege zake 12,” alisema Majaliwa bila kutaja bei iliyotumika kuzinunua ndege hizo.
Kampuni ya ndege ya Canada ya De Havilland inaeleza kuwa De Havilland zina uwezo wa kubeba abiria hadi 90 wakati Airbus A220-300 zina uwezo wa kubeba abiria hadi 150 kwa wakati mmoja.
Ujio wa ndege hiyo huenda ukaiongezea nguvu ya ushindani Shirika la ndege Tanzania (ATCL) kwa kupanua safari zake za ndege za ndani na kimataifa ili kuchochea shughuli za utalii, biashara na ajira.
Kwa sasa ATCL inachuana vikali na Shirika la ndege la Precision Air baada ya kampuni ya ndege ya FastJet kusitisha huduma zake miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, kumewa na maoni tofauti kuhusu ununuzi wa ndege miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wakieleza kuwa ununuzi wa ndege hauna tija kwa kuwa unailetea hasara Serikali. Wengine wanadai biashara hiyo iendelee ili kusaidia kukuza shughuli nyingine za kiuchumi hususan utalii.