November 24, 2024

Tanzania yapokea takriban Sh15 bilioni kupambana na Corona

Ni fedha zilizotolewa na taasisi tatu za Global Fund, Airtel Tanzania na Rotary Club Tanzania.
Sehemu kubwa ya msada huo utatumika kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya.

  • Ni fedha zilizotolewa na taasisi tatu za  Global Fund, Airtel Tanzania na Rotary Club Tanzania.
  • Sehemu kubwa ya msada huo utatumika kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa Sh14.9 Bilioni  kutoka kwa taasisi tatu za Global Fund, Airtel Tanzania na Rotary Club Tanzania na sehemu kubwa ya msada huo itatumika kununua vifaa tiba na kinga kwa ajili ya watumishi wa afya na kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya Corona ( #COVID19).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliyekuwa akipokea msaada huo leo (Aprili 27, 2020) jijini Dar es Salaam amesema kati ya fedha hizo, Global Fund imetoa Sh14 bilioni, Airtel Tanzania (Sh700 milioni) na Rotary Club Tanzania Sh250 milioni.

Amesema fedha hizo kwa sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya ambao wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 

“Tumepokea Sh14 bilioni kutoka Global Fund, Sh9.6 bilioni tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko,” amesema Ummy. 

Amesema kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda watumishi wa afya na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari na kuzingatia miongozo wakati wakitoa huduma ili kuepuka maambukizi.


Zinazohusiana


Waziri huo amesema ushiriki wa kila mdau katika mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kuwa msaada uliotolewa na kampuni hizo ni muhimu katika kutomeza virusi hivyo nchini. 

Mpaka sasa Tanzania imeripoti kuwa na wagonjwa  284 wa Corona huku 48 wakipona. Jiji la Dar es Salaam linaendelea kuwa kitovu cha ugonjwa COVID-19 kwa kuwa na wagonjwa 143 likifuatiwa na Zanzibar yenye wagonjwa 98.