Tanzania yaporomoka ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani
Wakati Tanzania ikiendelea kuwa kinara wa vivutio vya asili vya utalii Afrika, katika anga za kimataifa imeporomoka kutoka nafasi ya pili iliyoshikilia mwaka 2014 hadi nafasi ya 12 mwaka huu duniani.
Kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi ya watu katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili ni baadhi ya sababu zilizochochea kushuka kwa ubora wa vivutio vingi vya utalii vya asili. Picha| K15 Photos.
- Ni baada ya kushika nafasi ya 12 mwaka huu kutoka nafasi ya pili mwaka 2014.
- Bado inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na vivutio vingi vya asili.
- Uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya hifadhi vyachangia kushuka.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) imeitaja Tanzania katika nafasi ya kwanza Afrika na ya 12 duniani kwa ubora wa vivutio vingi vya utalii vya asili, jambo linaloiweka katika nafasi nzuri ya kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.
Ripoti hiyo inaangazia mazingira wezeshi kwa utalii, miundombinu, maliasili na utamaduni katika nchi 140 duniani.
Ripoti hiyo ya utafiti wa Ushindani wa Safari na Utalii kwa mwaka 2019 iliyotolewa na WEF imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi hizo kutokana na kuwepo kwa sera na mikakati mathubuti ya kulinda na kuendeleza rasilimali za asili ambazo zimekuwa zikihitajika zaidi katika kuvutia watalii.
Wakati Tanzania ikiendelea kuwa kinara wa vivutio vya asili vya utalii Afrika, katika anga za kimataifa imeporomoka kutoka nafasi ya pili iliyoshikilia mwaka 2014 hadi nafasi ya 12 mwaka huu duniani.
Hiyo ina maana kuwa Tanzania imeporomoka kwa nafasi 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dalili za Tanzania kuporomoka katika ubora wa vivutio vya utalii vya asili, zilianza kuonekana katika matokeo ya awali ya utafiti huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano ambapo alishika nafasi ya nane duniani.
“Lakini matokeo ya katikati ya utafiti huo ambao unafanyika kila baada ya miaka mitano yalitoka (na) Tanzania inaonekana imeshuka toka nafasi ya pili mpaka ya nane kwa vivutio vya nature (asili) duniani,” alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, akiwa bungeni Mei 21, 2019.
Dk Kingalla aliyekuwa akijibu swali la mbunge wa Vunjo, James Mbatia, alitaja sababu kubwa iliyosababisha Tanzania kushuka ni kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi ya watu katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili.
Zinazohusiana
- Tanzania yaporomoka kwa ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania
Hata hivyo, alibainisha kuwa kazi kubwa imefanyika katika Serikali ya awamu ya tano ya kuwaondoa wananchi ambao wamevamia maeneo hayo lakini pia kupandisha hadhi baadhi ya maeneo ya asili ili yahifadhiwe na kulindwa.
Pamoja na matokeo hayo, bado Tanzania inafanya vizuri katika maeneo mengine ya kuendeleza rasilimali za asili.
Ripoti hiyo, imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 10 duniani kwa uhifadhi wa maliasili na nafasi ya 18 kwa kuhifadhi na kuendeleza maeneo yake yaliyoorodheshwa katika maeneo muhimu ya urithi wa dunia ikiwemo pori la Akiba la Selous na mlima Kilimanjaro.
Ripoti hii inachapishwa kwa malengo ya kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, safari na kuwaleta pamoja viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta hii inafikia mahitaji ya miundombinu ya safari na utalii ya karne ya 21.
Pia inalenga kuwasaidia watunga sera kufahamu madhara mbalimbali yanayoweza kuibuka kutokana na sera hizo katika sekta ya utalii na safari hasa katika kufanya maamuzi na uwekezaji.