Tanzania yarekodi wagonjwa wapya 176 wa Corona ndani ya siku moja
Kiwango hicho ni kikubwa kutangazwa ndani ya siku moja tangu Serikali ianze upya kutoa takwimu Juni 28 mwaka huu.
- Kiwango hicho ni kikubwa kutangazwa ndani ya siku moja tangu Serikali ianze kutoa takwimu upya takwimu Juni 28 mwaka huu.
- Hadi Julai 21, kulikuwa na watu 29 waliofariki dunia.
Dar es Salaam. Tanzania imerekodi idadi kubwa ya wagonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19) ya watu 176 ndani ya siku moja, kiwango kinachofanya jumla ya waliothirika na ugonjwa huo kufikia 858.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa “hali siyo nzuri, haya tunayoyasema watu wayatekeleze.”
Kasi ya maambukizi ya wimbi la tatu la Uviko-19 imezidi kuongezeka ndani ya mwezi mmoja tangu Serikali ilivyoanza kutoa takwimu mpya Juni 28 mwaka huu huku Dk Gwajima akieleza kuwa sababu kubwa ni baadhi ya watu kupuuza miongozo ya afya kukabiliana na janga hilo.
“Kwa jana (Julai 22, 2021) pekee yake wagonjwa waliolazwa wapya hesabu yangu iliyonifikia inaniambia ni 176 nchi nzima,” amesema Dk Gwajima Ijumaa hii.
Jana waziri huyo katika taarifa yake kwa wanahabari alieleza kuwa hadi Julai 21 mwaka huu Tanzania ilikuwa na wagonjwa 682 wakiwa wameongezeka kutoka 408 walioripotiwa Julai 8. Kati ya kipindi hicho cha ndani ya wiki mbili jumla ya wagonjwa wapya 274 walibainika ikiwa ni sawa na wastani wa wagonjwa 21 kwa siku.
Hata hivyo, idadi ya wagonjwa wapya 176 iliyopotiwa ndani ya siku moja ni zaidi ya nusu ya wale walioripotiwa ndani ya kipindi chote cha siku 13 cha kati ya Julai 9 hadi Julai 21.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akizungumza na wanahabari Julai 23 mwaka huu kuhusu hali ya ugonjwa wa Uviko-19. Picha| Rayson Mwaisemba/ Wizara ya Afya.
“Ikumbukwe pia siyo kwamba watu hawafariki, la hasha wanafariki na kwa takwimu za 21 Julai hesabu yangu inaniambia watu 29 walifariki,” amesema waziri bila kubainisha kwa kina undani wa takwimu hizo.
Katika mkutano huo, Dk Gwajima amewasihi Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwa hiari bila kusubiria shuruti kutoka kwa mtu yeyote kwa kuwa ulegevu wao katika kujisimamia haukomoi mtu yeyote.
Aidha, Waziri huyo amewasihi Watanzania kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwemo ya kisiasa, ya kidini na hata ya kiburudani kwa kuwa vita dhidi ya Corona siyo ya Wizara ya Afya pekee bali ni ya Watanzania wote katika nafasi zao.
“Unapolazimika kuwa kwenye mikusanyiko, vaa barakoa, tumia vitakasa mikono, nawa mikono kwa maji na sabuni. Lazima wananchi na viongozi watimize wajibu wao,” amesema Dk Gwajima.
Aidha, Dk Gwajima amewasihi watu kuepuka taarifa za Corona zisizo rasmi kwa kuwa zinachochea wengi kupuuzia tahadhari za ugonjwa huo ambao unazidi kugharimu maisha mamilioni ulimwenguni.
Hadi jana Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa watu milioni 4.12 wamepoteza maisha ulimwenguni kwa Uviko-19 huku jumla ya visa vyote vikifikia milioni 191.8