November 24, 2024

Tanzania yashauriwa kutafakari upya kurejea mahakama ya Afrika

Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Jaji Sylvain Ore amesema anatazamia kuona utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ukiirejesha Tanzania katika mahakama hiyo.

  • Mahakama hiyo imesema inaamini Raised Samoa anaweza kuirejesha tena Tanzania.
  • Yasema itaendelea kushorikiana na Tanzania.

Dar es Salaam. Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Jaji Sylvain Ore amesema anatazamia kuona utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ukiirejesha Tanzania katika mahakama hiyo ili kuwapatia raia wake chombo huru cha kupata haki.

Tanzania ilijiondoa rasmi kwenye ibara ya 34(6) ya itifaki ya mahakama hiyo Novemba 2020 iyonayoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kupeleka mashauri yao kama hawajaridhika na maamuzi katika nchi zao.

Hiyo ni baada ya kupita mwaka mmoja tangu Tanzania kuiandikia barua AfCHPR kusudio la kujitoa.

Kanuni zinazoongoza mahakama hiyo zinaelekeza kuwa ikiwa kusudio la kujiondoa limedumu kwa mwaka mmoja, nchi inakuwa imejitoa rasmi katika mahakama hiyo.

Ore aliyekuwa akizungumza leo Mei 21, 2021 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu miaka 15 ya mahakama hiyo, amesema anatumaini Serikali ya Tanzania itafikiria upya uamuzi wake na itarejea tena katika mahakama hiyo.

“Kwa sasa, Tanzania ina utawala mpya chini ya Rais Samia Hassan, tunatazamia anaweza akafanya uamuzi mzuri wa kurudi na sisi tutaendelea kushirikiana naye,” amesema Ore.

Amesema Tanzania ni mdau muhimu katika maendeleo ya Afrika na imekuwa ikitoa ushirikiano kwa mahakama hiyo, hivyo bado kuna nafasi ya kuendelea kujadiliana kuhusu suala hilo.

Aidha, amesema Serikali ya Tanzania ina sababu za msingi kujitoa katika mahakama hiyo na hawezi kuingilia ila kuna umuhimu wa raia wake kupata chombo huru kitakachowahakikishia haki zao.


Soma zaidi: 


Wakati Tanzania inaripoti kuandika barua ya kujitoa katika itifaki hiyo Desemba 2019, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa wakati huo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Serikali ilichukua uamuzi wa kujitoa kwa muda katika itifaki hiyo kwa sababu haikuridhishwa na baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiendelea.

Hata hivyo, alisema Tanzania inaendelea kuwa mwanachama kwa sababu bado inaheshimu kipengele cha mwongozo wa uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, ni nchi 33 kati ya 55, wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ndiyo zimeridhia uanzishwaji wa mahakama hiyo ambapo kati ya hizo ni nchi tisa pekee zimekubali watu wake na mashirika binafsi kupeleka mashauri mbele ya mahakama hiyo.

Afisa Itifaki wa Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Tamambele Simba amesema sababu kubwa ya nchi zilizojitoa na ambazo hajiridhia itifaki ya watu wake kupeleka mashauri katika Mahakama ya Afrika ni kuogopa wingi wa kesi zinazofunguliwa ambazo wanafikiri zinatoa taswira mbaya katika jumuiya za kimataifa.

“Baadhi ya wakuu wa nchi wanaona suala hilo siyo zuri kwao kila mara kutajwa kwenye vikao vya wakuu wa nchi za AU kuwa kwa kushindwa kutekeleza maamuzi ya mahakama hiyo,” amesema Simba.

Mahakama hiyo ambayo makao yake makuu yako jijini Arusha inaadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake ambapo inafanya shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa wanahabari na kutembelea vyuo vikuu ili kuelezea kazi za mahakama hiyo.