October 8, 2024

Tanzania yatajwa nchi 10 zinazoongoza watoto kufariki kwa kichomi duniani

Ripoti mpya ya utafiti ya mashirika matano ya kimataifa likiwemo shirika la watoto duniani (UNICEF) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 duniani zilizokuwa na vifo vingi vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilivyotokana na ugonjwa wa kichomi

  • Imeshika nafasi ya 10 duniani ikiwa kundi moja na nchi zikiwemo za Angola na Chad.
  • Watoto 15,000 walio chini ya miaka mitano walifariki mwaka 2018.
  • Serikali, wadau wa afya watakiwa kuunganisha nguvu kutokomeza ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya utafiti ya mashirika matano ya kimataifa yanayohusika na masuala ya watoto likiwemo shirika la watoto duniani (UNICEF) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 duniani zilizokuwa na vifo vingi vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilivyotokana na ugonjwa wa kichomi kwa mwaka 2018. 

Kichomi ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria, virusi au fangasi na hufanya watoto kupata matatizo ya kupumua kutokana na mapafu yao kujaa usaha na maji.

Tanzania imeshika nafasi ya 10, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto 15,000 walifariki kutokana na ugonjwa huo nchini.

Hata hivyo, Nchi tano zilizohusika na idadi zaidi ya nusu ya vifo vyote vya kichomi duniani kwa mwaka jana ni pamoja Nigeria ambayo ilikuwa na vifo 162,000, India (127,000), Pakistan (58,000) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC (40,000) na 32,000 vilitokea Ethiopia. 

Nchi nyingine zilizoathirika na ugonjwa huu na kuingia katika orodha hiyo ni Indonesia, China, Chad, Angola na Tanzania.

Mashirika mengine yaliyoshiriki utafiti huo ni Ubia wa Chanjo duniani (GAVI), Save the Children, Every Breath Counts na Unitaid yanaeleza kuwa kwa mwaka jana pekee ugonjwa wa kichomi ulikatiza maisha ya watoto zaidi ya 800,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano sawa na mtoto mmoja kila sekunde 39.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN), utafiti huo umesema vifo vingi hutokea kwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili na takriban vifo 153,000 hutokea ndani ya mwezi mmoja wa maisha yao.

Ili kutoa tahadhari ya ugonjwa huo uliosahaulika, mashirika hayo matano jana (Novemba 12, 2019) yamezindua wito wa kimataifa wa kuchukua hatua ambao utafuatiwa na kongamano la kimataifa la ugonjwa wa kichomi utotoni litakalofanyika nchini Hispania mwezi Januari 2020.

“Kila siku karibu watoto 2,200 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki duniani kutokana na kichomi; ugonjwa unaotibika na kuzuilika, hivyo hatua imara za kimataifa na kuongeza uwekezaji ni muhimu kukabiliana na ugonjwa huu. 

“Ni kwa kupitia miradi ya gharama nafuu, kinga na matibabu kufikishwa waliko watoto walioathirika ndipo tutaweza kuokoa maisha ya mamilioni, ‘’ amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore katika taarifa hiyo. 

Kwa mwaka 2018 utafiti huo unasema watoto wengi zaidi wa chini ya umri wa miaka mitano walikufa kwa  kichomi kuliko ugonjwa mwingine wowote, mwaka ambao ulishuhudia vifo vya watoto 437,000 walio chini ya umri wa miaka mitano kutokana na ugonjwa kwa kuhara na vifo 272,000 vilivyotokana na malaria kwa watoto wa umri huo huo.

Jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo

UNICEF na wadau wengine wanasema ugonjwa huo unaweza kuzuiliwa kwa chanjo na kutibika kirahisi kwa dawa za gharama nafuu za viua sumu endapo watafanyiwa vipimo kwa umakini. 

Lakini mamilioni ya watoto hawapati chanjo na mtoto mmoja kati ya watatu wenye dalili za ugonjwa huo hawapati huduma muhimu za afya zinazostahili.

Kwa mujibu wa utafiti huo watoto walioathirika vibaya na kichomi wanaweza kuhitaji matibabu ya hewa ya oxijeni ambayo si rahisi kupatikana katika nchi masikini ambako watoto huhitaji huduma hiyo.

“Sasa umewadia wakati kwa serikali, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa, makampuni, na mashirika yasiyo ya kiserikali kujiunga pamoja kupambana na kichoni na kuwalinda watoto hawa,” amesema Fore. 

Mashirika hayo yamezitaka serikali katika maeneo yaliyoathirika zaidi kuunda na kutekeleza mkakati wa kudhibiti kichomi na kupunguza vifo vya watoto vitokanavyo na ugonjwa huo kwa kuboresha huduma za afya za msingi kama sehemu ya huduma za afya kwa wote.