October 8, 2024

Tanzania yathibitisha kisa cha kwanza cha Corona

Tanzania inakuwa nchi ya tatu ya Afrika Mashariki kuthibitisha kuwa na mgonjwa wa virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi duniani.

  • Mgonjwa huyo ni Mtanzania ambaye amesafiri kutoka Ubelgiji.
  • Kwa sasa mgonjwa huyo anafanyiwa matibabu kwenye hospitali ya Mount Meru Arusha.
  • Inakuwa nchi ya tatu Afrika Mashariki kuwa na mgonjwa wa virusi vya Corona.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kuwepo kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona nchini Tanzania. 

Tanzania inakuwa nchi ya tatu ya Afrika Mashariki kuthibitisha kuwa na mgonjwa wa virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi duniani.

Mwalimu ambaye aliyekuwa akizungumza leo (Machi 16, 2020) jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari amesema mgonjwa huyo ni mwanamke mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili Tanzania jana Jumapili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Ubelgiji.

Hata hivyo, Ummy amesema mgonjwa huyo alifanyiwa vipimo akiwa uwanjani hapo lakini hakugundulika kuwa na homa.

Lakini, mara baada ya kutoka uwanjani hapo, mwanamke huyo alianza kujisikia vibaya akiwa hotelini na ndipo akaenda hospitali ya mkoa ya rufaa ya Mount Meru jijini Arusja Arusha ambapo sampuli iliyochukuliwa na kupelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii jijini Dar es salaam ilibaini kuwa ana maambukizi ya virusi vya Corona.

Amesema msafiri huyo aliondoka nchini Machi 3, 2020 ambapo kati ya Machi 5 hadi 13 alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji.


Zinazohusiana


Hata hivyo, Waziri huyo amesema mgonjwa huyo anaendelea na matibabu huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua kwaajili ya kuhakikisha ugonjwa huo hausambai nchini.

“Habari njema ni kwamba mgonjwa ni Mtanzania ila ametoka nje, ugonjwa haujaanzia Tanzania,tunawafuatilia wote waliokutana nae tangu jana alipofika uwanja wa ndege KIA tutawaweka katika nyumba za uangalizi kwa siku 14 ili kuhakikisha tunaidhibiti corona,” amesema Ummy.

Bunge la Tanzania nalo lachukua hatua

Bunge la Tanzania limesitisha safari zote za kikazi nje ya Nchi hadi itakapoamriwa vinginevyo ambapo taarifa ya Ofisi ya Spika wa Bunge imeeleza kuwa safari za matibabu nje ya Nchi kwa wanaogharamiwa na Bunge hasa kwenye nchi zenye wagonjwa wa Corona zitasitishwa kwa muda.

“Utaratibu wa kupokea Wageni wengi ikiwemo makundi ya Wanafunzi au Wananchi wanaotembelea Bunge kwa lengo la kuona au kujifunza Shughuli za Bunge utasitishwa kwa muda hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo. Wageni watakaoruhusiwa kuingia Bungeni ni wale wenye kazi au shida mahsusi,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Wabunge au watumishi wa Bunge waliotoka katika safari za nje ya nchi, watahitajika kupitia katika zahanati ya Bunge kujiridhisha kama wapo salama kabla ya kuendelea na majukumu yao ya kila siku bungeni.