November 24, 2024

Tanzania yathibitisha mgonjwa mwingine wa Corona

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona imefikia 13 baada ya mgonjwa mwingine kubainika kupata maambukizo ya ugonjwa huo.

  • Sasa ina wagonjwa 13, nane ni Watanzania na watano ni raia wa kigeni.
  • Yupo mgonjwa kutoka mkoani Kagera ambaye ni dereva wa magari makubwa.
  • Mgonjwa wa kwanza apona, Waziri Ummy aagiza asitengwe wala kunyooshewa kidole. 

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona imefikia 13 baada ya mgonjwa mwingine kubainika kupata maambukizo ya ugonjwa huo.

Ummy amesema licha ya kuwa idadi ya wagonjwa imeongezeka, hakuna kifo hata kimoja kilichoripotiwa na wagonjwa wa ugonjwa huo wanaendelea kupata matibabu.

Waziri huyo aliyekuwa akitoa taarifa kwa umma leo (Machi 26, 2020) ya maendeleo ya ugonjwa huo, amesema kuwa mgonjwa mmoja alipatikana mkoani Kagera na ni dereva wa magari makubwa, ambaye aliingia nchini kupitia mpaka wa Kabanga na shughuli zake anafanyia kati ya Burundi, DRC na Tanzania.

Amesema kati ya wagonjwa 13, nane ni Watanzania na watano ni raia wa kigeni. Wagonjwa hao nane wako katika jiji la Dar es Salaam, Arusha (2), Zanzibar (2) na mmoja yuko Kagera.

“Mgonjwa wa ndani alipata maambukizi kutoka kwa mtu aliyekua nje ya nchi, hivyo hadi sasa hakuna maambukizi ya ndani (Local transmission). Wagonjwa wote wanaendelea vizuri na nina furaha kutangaza kuwa Isabella amepona COVID19 baada kupimwa mara 3,” amesema Waziri Ummy. 

Wagonjwa waliopata ugonjwa huo 12 walisafiri nje ya nchi na mmoja hukusafiri kabla hajapata ugonjwa huo.

Pia ameiomba jamii kutowatenga watu waliobainika kuwa na virusi vya COVID19 kwani baada ya kuwekwa karantini na kupata huduma wanapona na wataruhusiwa kurudi mtaani, hivyo wasinyooshewe vidole na kunyanyapaliwa.

Ummy ametoa wito huo baada ya kutangaza kuwa mgonjwa wa kwanza wa Corona Isabella Mwampamba kuwa amepona na ataruhusiwa kwenda nyumbani.


Zinazohusiana


Hata hivyo, Serikali imeimarisha shughuli za upimaji katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege na watakaogundulika na ugonjwa huo wanawekwa karantini kwa siku 14. 

Ummy amesema kuanzia Januari hadi sasa jumla ya wasafiri Milioni 1.8 wamefanyiwa ukaguzi kwa kupimwa joto la mwili, huku wasafiri 111 wametengwa kwenye Hoteli na maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili yao ili wasichangamane na wenyeji kabla ya kufanyiwa vipimo.