November 24, 2024

Tanzania yatoa mwelekeo kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi

Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua ya mbalimbali kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje ya Tanzania ikiwemo kuwaelimisha Watanzania kuthamini bidhaa za ndani ili kuimarisha na kukuza viwanda vya ndani.

  • Yawataka Watanzania kuachana na dhana potufu kuwa bidhaa za nje ndizo zenye ubora.
  • Yawataka wathamini na kutumia malighafi za ndani kuongeza uzalishaji viwandani.

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua ya mbalimbali kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje ya Tanzania ikiwemo kuwaelimisha Watanzania kuthamini bidhaa za ndani  ili kuimarisha na kukuza viwanda vya ndani. 

Pia hizo ni pamoja na mafuta ya kula ambayo yamekuwa yakiingia nchini kufidia upungufu wa bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya nyumbani. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza Oktoba 7, 2019 wakati akifungua maonyesho ya Sido Kitaifa katika Manispaa ya Singida, amewataka Watanzania wanaofikiri kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora, kuachana na dhana hiyo potofu, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, bidhaa zetu ni nzuri na zinapendwa na watu wengi hata wa nje ya nchi. Mnachotakiwa kukifanya ni kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo yenu, hii itawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko,” amesema Majaliwa.  

Amesema wakizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi za ndanii itawezesha kupatikana kwa ajira endelevu kwa vijana, itasaidia malighafi kutoharibika lakini pia bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na thamani kubwa badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuifikisha Tanzania  kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Amesema uanzishwaji wa viwanda umejikita zaidi katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na maliasili inayopatikana nchini kwa sababu ndiyo njia sahihi kuelekea uchumi wa viwanda.  

“Kwa misingi hiyo, usindikaji, uchakataji na uchenjuaji, vitachangia kupunguza upotevu unaotokea msimu wa mavuno, kuongeza ajira na thamani ya mazao kwa lengo la kuwapatia wazalishaji kipato,” amesisitiza Waziri Mkuu. 

Amesema uongezaji thamani unahitaji teknolojia (mashine na ujuzi), ili kukamilisha azma ya kuongeza uzalishaji viwandani.