July 1, 2024

Tanzania yatoa tahadhari ya mvua kubwa siku tano

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yasema mvua hiyo inaweza kusababisha athari mbalimbali.
Athari zinazoweza kujitokeza ni shida ya usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yasema mvua hiyo inaweza kusababisha athari mbalimbali.
  • Athari zinazoweza kujitokeza ni shida ya usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
  • Itanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na Zanzibar.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari  kunyesha mvua kubwa kwa siku tano inayoweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa shughuli za usafirishaji katika baadhi ya mikoa nchini. 

Mvua hizo zilianza kunyesha jana Aprili 11 na zitaendelea hadi Aprili 15, 2021 katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) na Tanga pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zinaweza kuleta athari kwenye makazi ya watu na shida katika usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji pamoja na ucheleweshwaji wa baadhi ya shughuli za usafirishaji,” imeeleza taarifa ya TMA iliyotolewa Aprili 11, 2021. 

Tayari mkoa wa Dar es Salaam tangu Aprili 11 umekumbwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali na kuchangia tatizo la miundombinu na foleni kubwa ya magari. 

Pia mvua hizo zitanyesha katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Lindi, Iringa, Njombe, Ruvuma na Mtwara.

Mvua hizo zinazonyesha katika maeneo yanayopata kipindi kimoja na vipindi viwili vya mvua kwa mwaka, pia zitanyesha katika mikoa ya Njombe, Kagera, Geita, Mara, Mwanza, Kigoma na Katavi.


Zinazohusiana


“Tafadhali zingatia na ujiandae,” inaeleza taarifa ya TMA ambayo inasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka hiyo kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye shughuli zao.

Menejimenti ya maafa, watoa huduma za dharura pamoja na wadau wengine wanatakiwa kuchukua hatua za kuweka mipango stahiki kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.