July 8, 2024

Tanzania yavibana vyuo vilivyochelewesha mikopo ya wanafunzi

Yavitaka vyuo ambavyo haviwapa wanafunzi wao fedha za kujikimu kufanya hivyo kabla ya Ijumaa Juni 5.

  • Yavitaka viwalipe fedha za kujikimu kufikia ijumaa Juni 5.
  • Yaridhishwa na tahadhari dhidi ya Corona vyuoni. 
  • Wananchi watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari maana Corona bado ipo. 

Dar es Salaam. Serikali imesema imeridhishwa na tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona inayochukuliwa na vyuo nchini Tanzania huku akivitaka vyuo ambavyo havijawapa wanafunzi wao fedha za kujikimu kufanya hivyo kabla ya Ijumaa Juni 5. 

 Vyuo vya ngazi zote pamoja wanafunzi wa kidato cha sita wameanza masomo Juni mosi baada ya agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mwezi uliopita kwa kuwa ugonjwa wa COVID-19 umepungua kwa kiasi kikubwa nchini. 

“Wizara imefanya kazi ya ufuatiliaji katika vyuo mbalimbali, hakika vyuo vimeitikia wito wa kufuata maelekezo ya wizara ya afya katika kuhakikisha vinaweka tahadhari (ya Corona) kwa ajili ya wanafunzi,” amesema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako 

Prof Ndalichako amesema ugonjwa huo bado upo hivyo lazima vyuo vichukue tahadhari ya kuwakinga wanafunzi na maambukizi kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya ili kuwapa fursa ya kusoma.

Aidha, amevitaka vyuo ambavyo mpaka sasa havijawalipa wanafunzi wao fedha za kujikimu kufanya hivyo mara moja kabla ya Ijumaa kwa sababu Serikali tayari imeshatoa fedha husika.  

Amesema Serikali ilitenga Sh122 bilioni kwa ajili ya fedha ya ada na kujikimu kwa wanafunzi wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) iliyotolewa kabla vyuo kufunguliwa. 

“Nitoe wito kwa vyuo ambavyo bado havijakamilisha kuwalipa wanafunzi fedha za kujikimu ikifika Ijumaa wanafunzi wote wawe wamepata fedha zao, hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha kufanya malipo kwa wanafunzi, fedha zipo tayari chuoni,” amesema waziri huyo katika hafla ya kukabidhi magari matatu kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.


Zinazohusiana


Amesema hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika kwa wanafunzi kutopata fedha mpaka sasa kwa sababu Rais Magufuli alitoa maagizo kuwa wanafunzi wapate fedha zao kwa wakati.

“Hili suala la kusema wanafunzi wanachelewa kusaini siyo kweli. Mtu ana njaa atakataaje kusaini? Na kama amesaini kwanini usubiri huyu ambaye ameshiba na hana njaa…suala la kutoa fedha kwa wanafunzi naomba vyuo hadi Ijumaa wanafunzi wawe wamepata fedha zao,” amesema. 

Magari hayo manne yaliyokabidhiwa NIT yamenunuliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wa kuleta mapinduzi ya elimu ya ufundi Afrika Mashariki ambapo Tanzania ilipata mkopo wa Sh175 bilioni.