October 6, 2024

Tanzania yawataka watu kuacha kujiachia vita dhidi ya Covid-19

Daktari huyo amesema kwa sasa nchi za jirani ziko kwenye wakati mgumu wa kukabiliana na Covid-19 ingawa hapa nchini wengi “wamerelax” (hawafuati kanuni za afya).

  • Katibu Mkuu wizara ya afya asema ni vema kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwa una tabia za kubadilika badilika.

Mwanza. Wakati ugonjwa virusi vya corona (Covid-19) ukiendelea kutesa mataifa mbalimbali ulimwenguni, Serikali ya Tanzania imewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kufuata kanuni za afya kwa kuwa unabadilika badilika kila wakati.

Tahadhari hiyo inakuja wakati kukiwa na jumla ya visa milioni 174.3 vya Covid-19 ulimwenguni huku watu takriban milioni 3.8 wakipoteza maisha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof Abel Makubi ameeleza leo jijini Dodoma kuwa baadhi ya wananchi wameanza kupuuza tahadhari dhidi ya ugonjwa huo zikiwemo za kunawa mikono na maji tiririka na sabuni, kupaka vipukusi (sanitizer) pamoja kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko mikubwa.

“Wakati ugonjwa huo unaripotiwa nchini, juhudi nyingi za kupambana zilionyeshwa ambapo kila sehemu kuliwekwa vifaa vya kunawia mikono, hospitalini, stendi za daladala na kwenye mikusanyiko mingine, lakini zoezi hilo kwa sasa halitiliwi maanani,” amesema Prof Makubi.

Kiongozi huyo, ambaye ni daktari wa binadamu kitaaluma, amesema kwa sasa nchi za jirani ziko kwenye wakati mgumu wa kukabiliana na covid-19 ingawa hapa nchini wengi “wamerelax” (hawafuati kanuni za afya).

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof Abel Makubi. Picha|Daily News. 

Prof Makubi amesema historia ya ugonjwa huo inabadilika badilika na kwamba iwapo watu watachukua tahadhari unapotea na wakipunguza unaibuka upya.

Kwa sasa sehemu kubwa ya mataifa ulimwenguni yanakabiliwa na wimbi la tatu la Uviko-19 huku madhara makubwa yakishuhudiwa zaidi katika mataifa ya India na Brazil.

Amezitaka taasisi za kiserikali kuendelea kutoa elimu na kuweka vifaa vya kunawia mikono lakini pia viongozi wa kidini waendelee kuwahamasisha waumini wao kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.

“Tahadhari ziendelee kutolewa lakini wasiwape hofu kwa kuwa washajua kuwa ugonjwa ni wa kuishi nao,” amesema.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliunda kamati ya wataalam wa afya iliyotoa mapendekezo ya namna Serikali itakavyoweza kukabiliana na Covid-19.

Miongoni mwa mapendekezo ya kamati hiyo iliyoongozwa na Prof Said Aboud ni kutoa chanjo ya corona kwa Watanzania kwa hiari na kuzingatia mazingira ya kitanzania katika kudhibiti ugonjwa huo katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia (lockdown) kama zinavyofanya nchi nyingine.

Kwa nyakati tofauti Rais Samia amesisitiza Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo unaotesa hadi mataifa tajiri ulimwenguni.

Tanzania haijaripoti takwimu mpya za corona tangu Mei 2021 huku WHO ikionyesha kuwa ni visa 509 tu vya corona viliripotiwa na vifo 21.