July 5, 2024

Tanzania yetu nzuri

Tanzania ndiyo nchi ya kwanza barani Afrika yenye vivutio vingi zaidi vya kitalii

Karibu Tanzania
Nchi ya amani iliyojaa maziwa na asali

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii kuanzia maeneo ya kihistoria (Mapango ya Amboni na mengineyo, Hifadhi ya wanyama ya pori ya Gombe katika mkoa wa Kigoma yenye Sokwe, miji ya Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar- mji Mkongwe na nchi ya marashi na viungo), Hifadhi za Taifa (Manyara, Serengeti, Mikumi, Seleous, Ngorongoro) na hifadhi nyingi za wanyama zenye wanyama na ndege wa aina mbalimbali. 

Milima iliyopo kama vile mlima Meru, na mlima wenye volkano wa Oldonyo Lengai na mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, Kreta ya Ngorongoro na Bonde la Olduvai linalosemekana kuwa ni chimbuko la binadamu wa kwanza. Tanzania iko katika eneo zuri la kijiografia lenye mwambao mrefu wa pwani kwa ajili ya biashara ya kimataifa (zikiwemo fukwe mpya zinazojitokeza) kwa kuwa inahudumia nchi sita za bara zisizo na bandari. 

Pia imezungukwa na maziwa makuu ya Tanganyika, lenye kina kirefu zaidi barani Afrika, Ziwa Victoria ambalo ni miongoni mwa maziwa makubwa duniani- lenye wingi wa samaki wa maji baridi na Ziwa Nyasa lililopakana na Malawi. 

Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua haraka sana nchini Tanzania na kuongoza kwa kuchangia pato la Taifa (GDP) na pia ni miongoni mwa sekta zinazoongoza katika kuliingizia taifa fedha za kigeni.