October 6, 2024

TCAA yazikomalia Embraer 190 za Fastjet mpaka itakapolipa madeni

Uongozi wa TCAA wasema ndege aina ya Embraer 190 iliyokodiwa baada ya Fastjet kufungiwa haitaruhusiwa kuondoka nchini mpaka Fastjet walipe madeni wanayodaiwa.

Ndege za Fastjet zimekuwa zikisifika kwa kutoza nauli ndogo ukilinganisha na mashirika mengine ya ndege nchini, lakini linabiliwa na changamoto za utendaji na madeni. Picha|Club of Mozambique


  • Imesema haitafuta usajili wa ndege mbili aina ya Embraer 190 zilizokodiwa na kampuni ya Fastjet kutoa huduma ya usafiri nchini mpaka kampuni hiyo ilipe madeni yote inayodaiwa. 
  • Yasisitiza kuwa itaendelea kutekeleza sheria zinazosimamia usafiri wa anga bila ubaguzi ili kuendeleza ushindani katika sekta hiyo.
  • Ndege aina ya Embraer 190 iliyokodiwa baada ya Fastjet kufungiwa haitaruhusiwa kuondoka nchini mpaka Fastjet walipe madeni wanayodaiwa.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema hawataruhusu kuondoka nchini wala kuzifutia usajili ndege mbili aina ya Embraer 190 zilizokuwa zinatumika na kampuni ya Fastjet kutoa huduma ya usafiri nchini mpaka kampuni hiyo itakapomaliza kulipa madeni yote inayodaiwa. 

Ndege hizo,  zilizoingizwa nchini mwaka 2016 baada ya kampuni hiyo kuamua kuachana na matumizi ya ndege aina Airbus A319, zinatakiwa kurudishwa kwa mmiliki wake baada ya Fastjet kudaiwa kushindwa kulipa madeni..

Embrear 190, zenye uwezo wa kubeba abiri 180 kila moja, zilikuwa mbadala kwa kampuni hiyo iliyopo katika matatizo ya kifedha kwa sasa kutokana na unafuu wake katika matumizi ya mafuta  na kutohitaji gharama za matengenezo ya mara kwa mara. 

Katika mkutano wake na wanahabari leo (Desemba 27, 2018), Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema hawataruhusu kuondoka nchini wala kuzifutia usajili ndege hizo mpaka madeni ya zaidi ya Sh6 bilioni ambayo Fastjet inaidaiwa yalipwe. 

Awali katikati ya mwezi huu, TCAA ilieleza kuwa Fastjet imepoteza sifa ya kuendelea kutoa huduma ya usafiri na kutoa notisi ya siku 28 ya nia ya kuifuta kabisa kampuni hiyo nchini kutokana changamoto za uongozi, kuzidiwa na madeni inayodaiwa na taasisi mbalimbali.

 “Zile ndege walikodi (Fastjet) kwa mwenyewe, sasa mwenyewe amekataa halipwi ana madeni. Fastjet ana madeni kwa mkodishaji halipi…kwa hiyo mkodishaji akasema kwamba ndege zake zirudi kwake kwa maana ziondoke ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Johari na kuongeza;

“Lakini sisi kama Mamlaka ya Usafiri wa Anga tukawajibu haziondoki ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa sababu zimezaa madeni.”


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, haijawa bayana kuwa Fastjet ilizikodi ndege hizo kutoka katika kampuni gani ya ndege duniani.

Johari amesema baada ya ndege hizo kukodiwa zilisajiliwa Tanzania kwa namba 5H na mwenye mamlaka kisheria kufuta usajili huo ni Mkurugenzi Mkuu wa TCAA. 

“Lakini sheria inasema kwa mujibu wa kifungu cha 10 (i) inasema tutafuta usajili wa ndege ya Tanzania endapo madeni yote ya ndege hiyo yatakuwa yamelipwa,” amesema Johari. 

Bosi huyo ameeleza kuwa hadi sasa ndege moja bado ipo nchini na nyingine ilipelekwa jijini Nairobi Kenya kwa sababu za kwenda kufanyiwa matengenezo. 

Licha ya ndege nyingine kuwa tayari ilishaondoka nchini, Johari amesema bado haijafutiwa usajili ili irudishwe kwa mmiliki wake hivyo mamlaka haitafuta hadi Fastjet ilipe madeni hayo.

Sanjari na kuzizuia ndege hizo, TCAA imekanusha taarifa zinazosambazwa mtandaoni kuwa Fastjet imezuiliwa kuingiza ndege nchini na kueleza kuwa kampuni hiyo bado haijatimiza masharti yote  iliyopewa ikiwemo kulipa madeni na kumwajiri ‘Accountable Manager’ (Meneja mwajibikaji) mwenye uzoefu katika usafiri wa anga.

Tamko hilo la TCAA limekuja siku chache baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet Tanzania, Lawrence Masha kuliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa wamezuiliwa kuingiza ndege ya kukodi aina ya Boeing 737-500 baada ya ndege za awali kuzuiliwa mpaka madeni yalipwe.

Katika taarifa za awali zilizotolewa na Masha ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani zilieleza kuwa ndege hizo mbili ambayo moja iliwahi kukataliwa na TCAA zingeingia nchini Desemba 22, 2018. 

Johari ameweka wazi kuwa taarifa za Fastjet kuleta ndege hizo wamepata Desemba 24 zikiambatana na barua ya kumteua Masha kuwa Accountable Manager ambapo maombi hayo yanafanyiwa kazi na majibu yatatolewa wakati muafaka. 

Akizungumzia madai ya Fastjet kuamuriwa iondoke nchini, Johari amesema kinachoweza kuindoa kampuni hiyo ni matatizo ya kiungozi ambayo yanatakiwa kushughulikiwa kabla notisi haijasha la sivyo watasimamishwa kama walivyofanya kwa Air Tanzania mwaka 2008 baada ya kukiuka taratibu za usafiri. 

“Tutaendelea kufanya kazi kuhakikisha kuna ushindani katika sekta, kuhakikisha mashirika yote bila kubagua yanafuata masharti tuliyoweka kwa mujibu wa sheria,” amesema Johari.

Hata hivyo, amesema  Fastjet wameanza kulipa madeni inayodaiwa likiwemo la Sh760 bilioni kwa TCAA lakini bado hawajamalizia kulipa Dola za Marekani 156,000 (zaidi ya Sh355 milioni) na fedha zingine zinazodaiwa na watu tofauti tofauti. 

Fastjet ikikamilisha kulipa madeni yote bado itakuwa na kibarua cha kusubiri maamuzi ya TCAA iwapo itakuwa imetimiza masharti mengine iliyopewa ikiwemo kuwa na andiko linalothibitisha uwezo wa kifedha kuendesha kampuni na ndege za uhakika. 

Hivi karibuni wachambuzi wa masuala ya usafiri wa anga waliiambia Nukta kuwa kuondoka kwa Fastjet kutairejesha nchi katika zama za shirika moja kuhodhi biashara ya usafiri wa anga linaloweza kupandisha bei za tiketi na kuwaumiza abiria ambao wameanza kuonyesha muamko wa kutumia ndege. 

Shirika la Fastjet lilianza kupata changamoto za kifedha baada ya mmiliki wa awali Fastjet PLC aliyekuwa na asilimia 49 kujiondoa ambapo shirika hilo liliuzwa kwa wawekezaji wa ndani.

(Habari hii imeboreshwa leo Desemba 28, 2018 kwa kuongeza chati)