October 6, 2024

TCRA haitaongeza muda wa kupokea taarifa za waliolipia chaneli za bure

Baadhi ya wateja wa visumbuzi vya DSTV, ZUKU na AZAM TV wamesema hawakupata wito huo licha ya kulipia chaneli za bure.

  • Mwisho wa kuwasilisha taarifa hizo ni leo (Septemba 24, 2018).
  • Yasema muitikio wa watu kuwasilisha taarifa na matumizi yake yatatangazwa hapo baadaye.
  • Baadhi ya wateja wa visumbuzi vya DSTV, ZUKU na AZAM TV wamesema hawakupata wito huo licha ya kulipia chaneli za bure.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeweka wazi kuwa haitaongeza muda wa kupokea taarifa za wateja walionunua visimbuzi vya DSTV, Azam na Zuku na kulipia kutazama channeli za televisheni zisizo za kulipia.

Septemba 6 mwaka huu TCRA ilitoa muda wa hadi Septemba 24, 2018 kwa watumiaji wa visimbuzi hivyo vitatu kuwasilisha taarifa zao kwa mamlaka hiyo ili zifanyiwe kazi. Chaneli zisizo za kulipia ni TBC 1, ITV, STAR TV, CHANNEL TEN, EAST AFRICA TV na CLOUDS TV.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala amesema watu wanaendelea kupeleka taarifa zao na mamlaka hiyo inaendelea kuzipokea  hadi muda uliowekwa utakafika mwisho na haikusudii kuongeza muda mwingine tena.

Mwakyanjala ameiambia Nukta kuwa muitikio wa watu umekuwa wa kuridhisha, japokuwa hakuweka wazi matumizi ya taarifa hizo na zoezi likikamilika mamlaka hiyo itatoa  ufafanuzi wa kina.

“Hizo taarifa nadhani ilikuwa kwa ajili ya matumizi ya ofisi. mwisho ukipita tutawasiliana vizuri,” amesema Mwakyanjala.


Zinazohusiana: 


Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya muda wa mwisho wa kuwasilisha taarifa kutimia, baadhi ya watumiaji wa visimbuzi vya DSTV, AZAM TV na ZUKU wamesema hawakupata wito kutoka TCRA licha ya kuwa miongoni mwa watu waliolipia chaneli hizo na wanataka kurudishiwa pesa zao.

Mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es salaam, Sise Christopher (23) anayetumia kisimbuzi cha AZAM TV amesema hakupata wito wa kuwasilisha taarifa yeyote kutoka mamlaka hiyo.  

Wateja hao wanatakiwa kuwasilisha taarifa zenye jina la mtazamaji kama lilivyosajaliwa, aina kisimbuzi anachotumia, nambari ya kisimbuzi, nambari ya kadi ya kisimbuzi na eneo analoishi. Pia anatakiwa kuwasilisha kiasi cha pesa anacholipa kila mwezi na idadi ya miezi aliyolipia chaneli hizo za bure.

Naye mkazi wa Sinza, Jijini Dar es Salaam, Elizabeth Joachim hadi leo ambayo ni siku ya mwisho ya kuwasilisha taarifa TCRA, hajawahi kupata tetesi zozote za zoezi hilo tangu lianze.  

“Mimi ninatumia DSTV ila inawezekana ujumbe haujaja kwangu,” amesema Joachim

Taarifa hizo zinatakiwa ziifikie TCRA kwa barua pepe (e-mail) au barua ya kawaida kwenye anuani inayopatikana kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.

Ikumbukwe kuwa Agosti 14 mwaka huu (2018), Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Makyembe aliingilia kati sintofahamu iliyojitokeza kati ya TCRA na kampuni za visimbuzi za DSTV, ZUKU na AZAM TV na kuzitaka zifuate sheria na miongozo ya leseni zao na  kuacha kufanya mambo kwa kujificha.

Pia alinukuliwa akisema wanaangalia uwezekano wa kupata ushauri kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali namna ya kuwasaidia kuWArejeshea pesa watu ambao wamelipia chaneli za zisizo za kulipia.