November 24, 2024

TCU yaeleza sababu kuvifuta vyuo tisa Tanzania

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta hati za usajili wa vyuo vikuu vishiriki vitano, vyuo vikuu vitatu na chuo kikuu kishiriki kimoja baada ya kujiridhisha kuwa vyuo hivyo havina uwezo wa kujiendesha hata vikipewa muda zaidi.

  • Yasema vyuo hivyo  havina uwezo wa kujiendesha hata vikipewa muda zaidi.
  • Kati ya vyuo 19 vilivyotakiwa kufanya marekebisho, vyuo vinane vilifanikiwa na kuruhusiwa kuendelea na udahili. 
  • Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) kimeendelea kuziwa kufanya udahili kutokana na kutokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta hati za usajili wa vyuo vikuu vishiriki vitano, vyuo vikuu vitatu na chuo kikuu kishiriki kimoja baada ya kujiridhisha kuwa vyuo hivyo  havina uwezo wa kujiendesha hata vikipewa muda zaidi.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo (Januari 21, 2020) jijini Dar es Salaam, amevitaja vyuo vishiriki vilivyofutwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Jacob (AJUCO), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kadinali Rugambwa (KARUMUCo), Chuo Kikuu cha Teofile Kisanji (Teku-Dar es Salaam), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kituo cha St Marko na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo tawi la Arusha (JKUA).

TCU pia imefuta hati za usajili wa vyuo vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JOKUCo), Chuo Kikuu cha Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB)

Amesema tangu mwaka 2017, vyuo hivyo vilitakiwa kufanya maboresho mbalimbali lakini havikufanikiwa kurekebisha dosari hizo na hata vikiongezewa muda havitaweza kuboresha mazingira ya elimu.

“Licha ya tume kutoa ushauri na mafunzi mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kufundishia, pamoja na muda wa kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali kwa zaidi ya miaka mitatu, baadhi ya vyuo havikufanikiwa,” amesema Prof. Kihampa.


Zinazohusiana: 


Amesema kati ya vyuo 19 vilivyotakiwa kufanya marekebisho, vyuo vinane vilifanikiwa na kuruhusiwa kuendelea na udahili.

Vyuo vilivyoruhusiwa kufanya udahili kwa baadhi ya masomo ni Chuo cha Umoja wa Waafrika Tanzania, Teofilo Kisanji (Mbeya), Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo na Chuo Kikuu cha Kampala-Tanzania.

Vingine ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian, Chuo Kikuu Kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia cha St. Joseph, Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCo) na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo)

Aidha, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema Chuo Kikuu Kishiriki na Sayansi Shiriki cha St. Francis cha Ifakara (SFUCHAS) kimeruhusiwa kufanya udahili kuanzia mwaka 2020/21.

Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) cha Lushoto mkoani Tanga kimeendelea kuziwa kufanya udahili kutokana na kutokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.