October 6, 2024

Teknolojia inavyotumika kuokoa mazingira

Huusisha matumizi ya nishati mbadala, vifaa vya kielektroniki na urejelezaji wa taka ili kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.

  • Huusisha matumizi ya nishati mbadala, vifaa vya kielektroniki na urejelezaji wa taka ili kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.
  • Wadau washauri elimu na hamasa ya kuhifadhi mazingira itolewe kwa watu. 

Lengo la matumizi ya teknolojia ni kurahisisha mahitaji muhimu kwa binadamu katika kufanikisha hali inakuwa nzuri kuliko ilivyokuwa awali  katika sehemu mbalimbali.

Wabunifu kwa nyakati tofauti wamekuwa wakibuni teknolojia rahisi zinazoweza kutumika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuhakikisha ustawi mzuri wa binadamu.  

Nukta tunakuletea teknolojia mbalimbali zinazotumika kutunza mazingira na kuhakikisha dunia inakuwa sehemu nzuri ya kuishi. 

Matumizi ya Nishati Mbadala

Nishati mbadala ni chanzo chochote cha nishati ambacho ni mbadala kwa mafuta ya visukuku. Ni nishati ambazo hazikaushi rasilimali za dunia na hazichafui mazingira.

Idris Hamis, mkazi wa Tabora ni miongoni mwa wabunifu wa nishati mbadala, amepata umaarufu kupitia mtandao wa kijamii kutokana na ubunifu wake wa kutengeneza mkaa huo kwa kutumia mabaki ya mazao pamoja na maranda ya mbao.

Pia matumizi ya unga wa muhogo katika utengenezaji wa mkaa mbadala unaotoa nishati bora ya kupikia na inayodumu kwa muda mrefu kuliko mkaa unaozalishwa na miti.

Novemba 4, 2017 wakati akihojiwa katika kipindi cha Njoo Tuongee, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba alieleza kuwa teknolojia ya nishati mbadala ni njia sahihi ya kupunguza tatizo la ukataji miti kwasababu imefanyiwa utafiti na kuonyesha matokeo chanya katika maeneo mbalimbali duniani.

“Teknolojia ni jawabu la uhifadhi wa mazingira, huo ni mwanzo tu wa utafiti wa utumiaji na usambazaji wa teknolojia”, alisema Waziri Makamba.

 

Matumizi ya nishati jadidifu

Nishati jadidifu hujumuisha umemejua, maji na jotoardhi na upepo ambao ni rafiki kwa mazingira hasa katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaathiri mwenendo wa maisha ya mwanadamu. Vyanzo hivyo ni endelevu na vinamuhakikishia mtumiaji upatikanaji wa umeme wakati wote.

“Gharama za umeme zinaweza kupunguzwa ikiwa tutageukia nishati jadidifu,” amesema Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi.

Matumizi ya nishati jadidifu kutumiza zaidi vijijini lakini yanajipatia umaarufu maeneo ya mijini hasa katika hoteli na taa za kuongoza magari ili kuboresha huduma za kijamii.


Zinazohusiana: 


Teknolojia ya kubadilisha taka ngumu kuwa sehemu ya mapambo

Taka hizo ni pamoja na chupa ya plastiki, matairi ya magari na chupa mbalimbali za vinywaji vikali au mvinyo zinabadilishwa na kuwekewa nakshi pamoja na kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya biashara. 

Mmoja wa wajasiriamali hao ni Irene Muja ambaye anamiliki kampuni ya Mabaki Mali ambaye anatumia matairi ya magari kutengeneza makochi na meza za mapambo ya nyumbani ikiwa ni hatua ya kupunguza uchafuzi wa mazingira. 

“Tumefanikiwa kusafisha zaidi ya matairi 500 hapa jijini, kwa kukadiria tunakusanya Kg 200 za matairi kwa mwezi,” anasema Muja.

Muonekana wa meza ndogo za mapambo zilizotengenezwa kwa mabaki ya taka. Picha| Mabaki Mali.

Matumizi ya vifaa vya kielektroniki

Teknolojia ya kupunguza matumizi ya karatasi ni kutumia prgramu za kompyuta katika uhifadhi wa nyaraka. Teknolojia hii ni endelevu ambayo inasadia kupunguza ukataji wa miti na matumizi ya kuni.  

Matumizi ya vifaa vya kupunguza joto pia husaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, licha ya ukweli kwamba teknolojia haitumiwi na wananchi wa kipato cha chini kutokana na gharama kubwa upatikanaji.

Licha ya wabunifu kutumia teknolojia kupambana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira, elimu inapaswa kutolewa ili kubadili mtazamo na tabia za baadhi ya watu ambao hawana muamko wa kutunza mazingira katika maeneo yao.

“Sisi huwa tunafanya kampeni za Nipe Fagio kwa kuwashirikisha vijana na makampuni yanayofanya huduma za “recycling” (kurudisha taka katika hali ya mwanzo ili zitumike tena),” anasema Salha Aziz, balozi wa kampeni ya Nipe Fagio.