October 6, 2024

Teknolojia zitakazoboresha utendaji wa vyombo vya habari Tanzania

Vyombo vya habari vya Tanzania vimetakiwa kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo ndege zisizo na rubani katika kuongeza ufanisi wa uchakataji na usambazaji wa habari kwa wananchi wanaowahudumia.

  • Teknolojia hizo ni pamoja na visaidizi vya sauti, AR na VR.
  • Wadau wamesema bado safari ni ndefu japo kuna fursa zimejificha.
  • Vyuo vyashauriwa kutoa elimu ya ubobezi kwa wanahabari ili waandike habari wakiwa na uhakika nao.

Dar es Salaam. Vyombo vya habari vya Tanzania vimetakiwa kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo ndege zisizo na rubani katika kuongeza ufanisi wa uchakataji na usambazaji wa habari kwa wananchi wanaowahudumia. 

Hatu hiyo itasaidia wanahabari na vyombo vya habari kuwafikia wananchi kwa urahisi na wakati huo huo kuongeza mapato katika shughuli zao za kila siku. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema zipo teknolojia mbalimbali ambazo zimevumbiliwa nchini na nje ya nchi ambazo zikitumika kwa usahihi zinaweza kubadilisha namna wanahabari wanavyowasiliana na jamii inayowazunguka. 

Dausen alikuwa akizungumza leo (Machi 11, 2020) jijini Dar es Salaam katika mdahalo kuhusu suluhisho za kidijitali zinazoweza kutumiwa na tasnia ya habari Tanzania uliondaliwa na Mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF) kwa kushirikiana na Nukta Africa na Hamasa Magazine.

Amezitaja baadhi ya teknolojia hizo ambazo ni rafiki wa Watanzania kuwa ni pamoja na 

Mashine za Akili bandia (Artificial intelligence) na roboti za kuchati (Chatbots) ambazo zimekuwa zikitumika na vyombo mbalimbali vya kimataifa ambazo zinatumika katika uchambuzi wa habari. 

Pia teknolojia ya visaidizi vya sauti kwenye simu za mkononi, AR na VR(Augmented Reality and Visial Reality) ambayo inabadilisha uhalisia na kuuingiza kwenye mfumo wa kompyuta. Kupitia teknolojia ya simu janja unaweza kuona kuliona jiji la Dar esSalaam kidijitali.

VR ni teknolojia ambayo inafanya kazi kupitia kompyuta ambapo mazingira halisia yanahuishwa na kutumika katika kutengeneza maudhui.

“Kama Watanzania hatupo makini, mtu nje ya Tanzania anaweza kuja kuwekeza kwenye teknolojia hii na kutengeneza pesa nyingi sana,” amesema Dausen.


Soma zaidi:


Teknolojia nyingine ni majukwaa ya usambazaji pamoja na matumizi ya teknolojia ya ndege zisizo na rubani (Drone) ambayo inaweza kumpatia mwanahabari habari nyingi za uhakika.  

“Kupitia teknolojia hii, ninaona stori nyingi sana. Ninaona stori ambazo huwezi kuziona ukiwa kwenye daladala. Hizi ni vumbuzi ambazo zimekuwepo lakini havijatumika kikamilifu,” amesema Dausen.

Amesema teknolojia hizo zitasaidia vyombo vya habari kunuafaika kwa mapato pato kwani watapata nafasi za matangazo na kufahamika kimataifa kwa kuwa “tunakoelekea ni dijitali tu.”

Hata hivyo, ili teknolojia hizo zilete maana wanahabari wanapaswa kuongeza ubunifu katika kazi hasa kutengeneza habari zenye ubora wa hali ya juu.

Mkuu wa Uzalishaji wa kampuni ya Haak Neel Production Ltd, Hatibu Madudu amesema wanahabari wanapaswa kubobea katika uandishi wa habari za masuala ili kuwahabarisha wananchi habari zenye viwango vya juu. 

Amesema ni muhimu kwa vyuo vinavyofundisha wanafunzi wanaosomea uandishi wa habari kuongezewa uwezo kutumia mifumo ya teknolojia ili iwasaidia wakiingia kazini.