TMA yatumia tamasha la Urithi Festival kutoa elimu ya hali ya hewa Dar
Yaeleza kuwa taarifa sahihi za hali ya hewa ni muhimu katika uhifadhi mali kale na utamaduni wa Mtanzania.
- Mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kuongezeka kwa joto na kina cha bahari kinatishia uwepo wa vivutio vinavyopatikana pwani ya bahari.
- Sekta ya utalii imetakiwa kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa ili kuhakikisha mali kale na vivutio vya utalii nchini vinatunzwa na kuendelezwa na kuwa sehemu ya kuenzi urithi na utamaduni wa Mtanzania.
Dar es Salaam. Sekta ya utalii imetakiwa kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa ili kuhakikisha mali kale na vivutio vya utalii nchini vinatunzwa na kuendelezwa na kuwa sehemu ya kuenzi urithi na utamaduni wa mtanzania.
Hali hiyo imejitokeza kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kuongezeka kwa joto na kina cha maji ambacho kinatishia uwepo wa mali kale zinazopatikana maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano cha Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) katika maadhimisha ya mwezi wa Urithi Festival kwa mkoa wa Dar es Salaam yanayofanyika kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama kuanzia Oktoba 1 hadi 6, 2018, inaeleza kuwa taarifa za hali ya hewa zinasaidia kuchukua tahadhari na kutunza urithi wa nchi na vivutio vya utalii.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi tafiti zinaonesha uwepo wa ongezeko la kina cha bahari hivyo kupelekea uwezekano wa kupotea kwa majengo ya zamani yaliyo kando ya fukwe za bahari.
Aidha, mabadiliko hayo husababisha kuhamahama kwa wanyama kutokana na kutafuta malisho, ikumbukwe kuwa uoto wa asili hutegemea hali ya hewa nzuri kama vile mvua za kutosha.
“Miongoni mwa elimu inayotolewa ni matumizi ya taarifa za hali ya hewa za muda mfupi, kati, mrefu na takwimu za hali ya hewa katika kulinda mali kale mfano majengo ya zamani yaliyo kando ya fukwe za bahari,” inaeleza taarifa hiyo.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Mama Samia atoa maagizo matano kukuza sekta ya utalii Tanzania.
Pia taarifa za hali ya hewa zinasaidia kuchagua vazi la asili la kuvaa kwa kipindi husika kama vile baridi, joto ili kuhakikisha watanzania wadumisha na kuendeleza mila na desturi za mavazi yao.
“Ngoma na michezo ya asili pia hutegemea hali ya hewa ya eneo husika kama vile upepo mkali, mvua kubwa kwa maeneo ya michezo ya ziwani, viwanjani,” inasomeka taarifa hiyo.
Maadhimisho ya mwezi au tamasha la Urithi Festival yalizinduliwa Septemba 15, 2018 na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma na yanatarajiwa kuhitimishwa Jijini Arusha; kitovu cha shughuli za utalii nchini.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Urithi Festival kwa mwaka huu linaadhimishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na visiwa vya Zanzibar ambapo shughuli zinazofanyika katika tamasha hilo ni ngoma na muziki wa asili, mapishi ya vyakula vya kitanzania, maonyesho ya zana za utamaduni na vivutio vingine vya utalii.
Kuanzia mwaka 2019, Tamasha hilo litakuwa linaadhimishwa katika mikoa yote na linatarajiwa kufungua fursa mbalimbali kwa kampuni za utalii kuwekeza katika maeneo mbalimbali na wananchi kupata ajira na uhakika kuendesha maisha yao.
Malengo ya Urithi Festival ni pamoja na kuimarisha, kuendeleza na kutangaza alama na tunu za Taifa ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo. Pia ni chombo muhimu ya kutangaza vivutio vya utalii na utamaduni wa Mtanzania ambao kwa muda mrefu haujatambulika katika nyanja za kimataifa.