July 8, 2024

TPDC yafungua fursa ya uwekezaji vituo vya gesi asilia Tanzania

Wajasiriamali wakaribishwa kujenga na kuuza gesi hiyo kwa watumiaji wa mwisho wakiwemo wamiliki wa magari yanayotumia nishati hiyo.

  • Wajasiriamali wakaribishwa kujenga na kuuza gesi hiyo kwa watumiaji wa mwisho.
  • Vituo hivyo vitakuwa vinauza gesi kwa wamiliki wa magari yanayotumia rasilimali hiyo. 

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefungua milango kwa wajasiriamali  na kampuni kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kuuzia gesi asilia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya magari yanayotumia nishati hiyo.

Wamiliki wa vituo hivyo watakuwa wananunua gesi hiyo kwa msambazaji mkuu na kuwafikishia watumiaji wa mwisho wakiwemo wamiliki wa magari yanayotumia gesi asilia. 

Kwa mujibu wa  tangazo lililotolewa TPDC kwa umma linaeleza kuwa  linatafuta mwekezaji atakayewekeza katika uchimbaji wa gesi na usambazaj gesi jijini humo kwa ajili ya magari.

“Kuanzia Julai Mosi TPDC itaanza kujenga mitambo mikubwa miwili katika jiji la  Dar es Salaam ambayo itasaidia usambazaji wa gesi (CNG) kwa vituo vidogo ambavyo vipo mbali na miundombinu ya bomba la mafuta,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo.


Soma zaidi: Statoil yaja kivingine uchimbaji wa gesi Tanzania


Mwekezaji anatakiwa kuonyesha nia ya dhati na ushaidi wa uzoefu wake na uwezo wa kufanya hiyo kazi ya kusimamia vituo vya kuuza gesi ili aweze kupatiwa leseni na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kwa mujibu wa sheria.

Licha ya kuonyesha nia, atawajibika kutoa taarifa zake za nyuma kuhusu kazi hiyo sambamba na muundo wa  wa uongozi katika kampuni yake.

Masharti mengine ni pamoja na kuwa na uwezo wa kifedha au utaratibu wa kutekeleza uwekezaji huo, kuhakikisha usalama wa umma ambapo mwekezaji anapaswa kuonyesha kuwa na ujuzi wa usalama wa afya na masuala ya mazingira kuhusiana na sekta ya mafuta. 

Pia utayari ya kutekeleza mpango wa maudhui ya ndani na masuala mengine ambapo atawajibika kusafirisha gesi hiyo kutoka mtambo mama hadi kituoni huku Ewura atabaki na jukumu la kupanga bei.