November 24, 2024

Trump adai hakuna tatizo Google kushirikiana na China

Amesema hakuna tishio lolote la usalama kwa kampuni hiyo kushirikiana na nchi ya China.

  • Amesema hakuna tishio lolote la usalama kwa kampuni hiyo kushirikiana na nchi ya China. 
  • Amesema kama kuna tatizo watalibaini tu. 

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema haoni kama kuna tishio la usalama kwa nchi yake kutokana na mahusiano yaliyopo kati ya kampuni ya teknolijia ya Google na China. 

Trump ametoa kauli hiyo leo (Julai 26, 2019) katika ukurasa wake wa Twitter, ambapo amesema kama kuna tatizo kwa China kushirikiana na Google watabaini.

“Na matumaini kuwa hakuna tatizo,” ameandika Trump.

Siku 10 zilizopita, Rais huyo alisema kuwa wataichunguza kampuni hiyo jinsi inavyoshirikiana na China katika masula mbalimbali ya teknolojia. 

Trump alifikia uamuzi huo baada ya mfuasi wake na mfanyabiashara wa Marekani, Peter Thiel kuyataka mashirika ya ujasusi ya nchi hiyo ya FBI na CIA kuichunguza kampuni hiyo kwa sababu inaweza kuwa inatumiwa na vyombo vya usalama vya China kuihujumu nchi yake. 

Hata hivyo, Msemaji wa Google, Riva Sciuto amekanusha madai hayo na kusema, “kama tulivyosema kabla, hatufanyi kazi na jeshi la China.” 

Wakati Trump akisema uhusiano wa Google na China hauna tatizo, Marekani bado imeiwekea ngumu kampuni ya simu ya Huawei kufanya kazi na makampuni yake kwa madai kuwa imekuwa ikiisaidia China kuingilia shughuli zake.